Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu: Dhahabu haijauzwa, matibabu yasitugawe

Muktasari:

  • Waziri amesema minong’ono hiyo haina ukweli kwani inatolewa na watu wenye chuki ambao ajenda zao ni kuwagombanisha wananchi na Serikali badala yake akaeleza uuzwaji wa dhahabu hauwezi na hautakuwa wa kificho kwani sera inataka itangazwe.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema hadi sasa ina akiba ya takribani tani 27 za dhahabu yenye zaidi ya thamani ya Dola 3 bilioni (sawa na Sh7.8 trilioni) ambayo ni asilimia 45 ya akiba na haijauzwa kama ambavyo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo Alhamisi Juni 18, 2026 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini (CCM) Esther Matiko ambapo amesisitiza uuzwaji wa dhahabu hauwezi kuwa wa kificho.

Katika swali lake kwa Waziri Mkuu, Matiko ametaka kujua kuhusu minong’ono ambayo inaeleza dhahabu ya Tanzania ambayo ilianza kununuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa utaratibu maalumu mwaka 2024, kuwa imeuzwa.

Katika majibu yake, Dk Mwigulu amesema minong’ono hiyo haina ukweli kwani inatolewa na watu wenye chuki ambao ajenda zao ni kuwagombanisha wananchi na Serikali.

 “Uuzwaji wa dhahabu hauwezi na hautakuwa wa kificho kwani sera inataka itangazwe kwenye gazeti na mnunuzi ajulikane.”

“Ni kweli hapo nyuma Serikali ilitaka kuuza dhahabu zake ili kuendelea na mfumo wa kununua zingine na hapo bei ilikuwa juu, lakini kutokana na machafuko huko duniani, bei ilishuka na kwa kuwa hatukuwa na kitu cha lazima cha kutafuta fedha, BoT waliamua kuachana nayo,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema ikitokea bei kuwa nzuri katika soko la dunia, Serikali itauza kwa utaratibu wa wazi na pesa zitakazopatikana zitakwenda kununua dhahabu nyingine kwa utaratibu wa kuhifadhi akiba kama ilivyo kwa akiba ya dola, ili linapotokea jambo, itusaidie.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza bungeni leo Alhamis Juni 18, 2026 wakati akijibu maswali ya wabunge.

Kingine Waziri Mkuu amesisitiza Serikali ina akiba ya kutosha kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu mbele hivyo akawataka Watanzania wasiwe na shaka na hata kama itauzwa haitauzwa kwa mtu binafsi.


Mjadala wa matibabu

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ni kama amezima moto wa wabunge kuhusu mivutano ya matibabu kwa pande mbili za Muungano ambapo ametaka kuwepo na utulivu, kwani hakuna jambo baya linaloweza kuwagawa.

Dk Mwigulu amekiri yapo mambo ya Muungano na yasiyokuwa ya muungano ikiwemo suala la afya, lakini akafafanua kuwa wizara mbili za afya zimekubaliana kupokea kadi za bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya Tanzania Bara na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) kwa Zanzibar.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza ambaye ameuliza Tanzania ni Jamhuri ya Muungano, lakini yapo masuala yasiyo ya Muungano ikiwemo afya, lakini hivi karibuni kumekuwepo na mijadala mikubwa kuhusu matibabu je, ni upi utaratibu wa kisera na kisheria unaotumika kuwahudumia Watanzania wa pande zote mbili kwenye maswala yasiyo ya Muungano?

Katika majibu yake, Dk Mwigulu amesema: “Ni kweli nami nimesikia mjadala huu na Mbunge umelileta kwa wakati, mpango ulipo ni kuwa kama utakuwa na kadi ya bima unaweza kutibiwa upande wowote wa Muungano na kama huna basi utatakiwa kulipa kwa taslimu.”

Hata hivyo, amekiri wapo wageni kutoka nje ya Tanzania ambao wamekuwa wakijipenyeza na kupata vibali vya ukazi ambao wanatumia fursa hiyo na hao ndiyo wanasababisha kelele hizo, ambapo amewataka Watanzania wazipuuze.

Dk Mwigulu amesema suala hilo lisitumike kuwagawa wananchi bali kutangaza fursa na mema yaliyopo kwani hata kero nyingi za Muungano zimefanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Mjini (CCM), Deodatus Mwanyika ameuliza ni lini Serikali itaanza kuwalipa wapiganaji waliopambana kwenye vita dhidi ya Uganda (1978/1979) ambao wamekuwa wakidai posho zao kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu amekiri jambo hilo limechukua muda mrefu lakini akataja sababu kuwa ilitokana na sheria za zilikuwa haziwatambui,  lakini wameshatambuliwa na uhakiki umeonyesha waliopo hai ni karibu 7,200.

Amesema kuanza mwaka ujao wa fedha Serikali itaanza kuwalipa kifuta jasho hicho hasa wale ambao hawakuwa kwenye majeshi lakini walikuwa wazalendo na wakaenda kuikomboa ardhi ya Tanzania.