Radi yaua wanafunzi sita Geita, 25 wajeruhiwa

Wazazi wa wanafunzi waliopigwa na radi wakiwa katika jengo la dharura wakisubiri kupewa taarifa za maendeleo ya watoto wao. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Tukio hilo la radi lilitokea saa tatu asubuhi na kusababisha vifo vya wanafunzi hao wa Shule ya Msingi Emaco Vision huku wengine wakiwamo walimu wao wakijeruhiwa


Geita. Wanafunzi sita wa shule ya msingi, Emaco Vision iliyopo mjini Geita wamefariki dunia baada ya kupiga na radi wakiwa darasani huku wengine wakijeruhiwa wakiwamo walimu wawili.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Oktoba 17, 2018  saa 3:30 asubuhi. Wakati mvua ikinyesha na radi kubwa kupiga.

Ofisa elimu msingi, Yese Kanyuma amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema hadi sasa majeruhi ambao bado wako hospitali ni 25.

Awali, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Octavia Laurian alisema madarasa yaliyopata kadhia ni ya darasa la kwanza hadi la tatu.

"Siwezi kusema kama kuna vifo maana sijathibitisha lakini waliokua na hali mbaya zaidi ni watatu na hawa 13 wana majeraha ya kawaida, wanafunzi wengi zaidi wamezimia" amesema Laurian.

Hadi sasa wazazi wapo kwenye viunga vya hospitali ya mkoa wakisubiri taarifa za watoto wao wanaopatiwa huduma kwenye kitengo cha dharura hospitalini hapo.