Richmond yageuzwa mtaji wa kisiasa

Dk Har

Muktasari:

GIRE WA RICHMOND AACHIWA HURU

Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Naeem Gire, ambaye alishtakiwa kwa tuhuma za kughushi na kuwasilisha serikalini nyaraka za kughushi katika sakata la Richmond, jana aliachiwa huru na  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka.

Hakimu Mfawidhi Cyprian Mkeha alimuachia huru jana Gire baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka mawili ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Hii ni mara ya pili kwa Gire, ambaye alikuwa wakala wa Richmond, kuachiwa huru na mahakama hiyo baada ya awali kumuona hana kesi ya kujibu.

 

Dar es Salaam. Kitendo cha viongozi wa Serikali kuendelea kuzungumzia sakata la mkataba wa Richmond, wakimuhusisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, limetajwa kuwa ni mtaji wa kisiasa.

Wachambuzi walioongea na Mwananchi pia wamesema Lowassa, ambaye aliihama CCM mwaka juzi na kujiunga na Chadema, hana budi kujitokeza sasa na kuanika ukweli.

Mwananchi ilifuatilia maoni ya wachambuzi baada ya sakata hilo kuibuka bungeni wakati wa mjadala wa hotuba mbili za bajeti za Ofisi ya Rais Tamisemi na Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambazo zilihitimishwa Alhamisi.

Sakata hilo linahusu mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya Richmond Development ya Marekani, ambayo ilionekana ilipewa zabuni wakati ikiwa haina uwezo.

Lowassa, ambaye alihusishwa na sakata hilo wakati akiwa Waziri Mkuu, alijiuzulu wadhifa wake na wakati wote amekuwa akieleza kuwa alipata maelekezo kutoka juu na kwamba aliwajibika kisiasa.

Lakini mara kadhaa, viongozi wa Serikali wamekuwa wakiibua na juzi Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata hilo, alisema yuko tayari kumuomba Rais John Magufuli amvue uwaziri iwapo wapinzani watalirejesha suala hilo bungeni, ili apambane nao.

Alisema hayo alipokuwa akijibu hoja za mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari aliyehoji sababu za Dk Mwakyembe kutomuhoji mteule wa Rais aliyeambatana na askari wenye silaha za moto, kuvamia studio za televisheni za kampuni ya Clouds Media.

Dk Mwakyembe ni mmoja wa wanasiasa ambao wamekuwa wakilizungumzia suala la Richmond katika majukwaa tofauti.

Jana, Lowassa hakutaka kuzungumzia kauli hiyo alipoulizwa maoni yake kuhusu kuibuliwa kwa sakata hilo.

“Sina kauli katika hilo,” alisema Lowassa.

Hata alipoulizwa sababu za kutoweka bayana kilichotokea, alijibu kwa kifupi akisema “sitaki kusema lolote bwana”.

 Katika mahojiano yake na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti, Lowassa amekuwa akitoa changamoto kwa Serikali akisema endapo kuna ushahidi wampeleke mahakamani na yeye atakuwa tayari.

Juzi, Nassari alisema katika sakata la uvamizi wa studio za televisheni za kampuni ya Clouds Media, Dk Mwakyembe hajatimiza ahadi yake ya kumuhoji mteule wa Rais anayehusishwa na uvamizi huo.

Akijibu hoja hiyo, Dk Mwakyembe alisema wapinzani wanataka kumsafisha Lowassa na kuwashauri waliwasilishe upya suala hilo bungeni na yuko tayari kuvuliwa uwaziri ili alishughulikie.

“Tunapochunguza, suala la kusikiliza upande mwingine upo wakati wa maamuzi, ndiyo maana sisi tulikuja hapa, tukaleta kazi hapa, tukiwa na mashahidi zaidi ya 40 wakitusubiri nje. Halafu leo unajifanya kuja kumsafisha?” alihoji Dk Mwakyembe.

“Huwezi kusafisha madoa ya lami kwa kutumia kamba ya katani au maji. Lileteni hili suala hapa tulimalize.”

Maoni ya wasomi, wanaharakati

Akizungumzia kujirudia kwa suala hilo,   mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho, alisema kuendelea kutaja jina hilo kunaweza kuwa mtaji wa kisiasa.

 “Wanafikiri inaweza kumuumiza (Lowassa) kisiasa. Mwanasiasa anapopata mwanya wa kumuumiza adui, anatumia nafasi hiyo,” alisema.

Pia, alisema inawezekana Waziri Mwakyembe ana imani kwamba sakata hilo litafufuliwa upya na kuchukuliwa hatua na Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na Serikali iliyopita kutochukua hatua.

Bunge lilifikia maazimio 23 ambayo Serikali ilitakiwa iyatekeleze, lakini haijatekeleza maazimio yote, likiwamo la kuwachukulia hatua watumishi wake waliohusika katika kashfa hiyo ambao kamati ilisema Lowassa alihusishwa kutokana na kutowasimamia vizuri.

“Wanasema jinai haifi na limechukua muda mrefu bila suluhu, hatukujua lilivyomalizika kama ilivyokuwa sakata la Escrow kwa hivyo pengine wanaamini kwamba wanaweza kuliibua upya ili lifanyiwe kazi,” alisema Profesa Shumbusho.

Mwanaharakati wa haki za binadamu na mtetezi wa masuala ya kijinsia wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali alisema kuna mchezo katika sakata hilo.

Gemma alisema Lowassa alishahoji  kuhusu kupelekwa mahakamani, lakini Serikali imebakia kuzungumza bila hatua zozote na badala yake wamekuwa wakimtuhumu tu.

Alisema hiyo ni sawa na mchezo wa “kupiga kamba kwenye maji”, akimaanisha ni mchezo wa kupiga kelele zisizokuwa na mwelekeo wa kupata suluhisho.

Alisema kushindwa kuchukua hatua dhidi ya Lowassa kunaonyesha kuna mipango ya kuwaficha wahusika wengine nyuma ya msalaba alioubeba Lowassa.

“Najiuliza kwa nini washindwe kumchukulia hatua sasa? Kwa sababu si kiongozi wa Serikali na hayuko CCM wala katika system (mfumo). Lazima kuna watu nyuma  ya ukimya huu na Lowassa anaonekana kula kiapo cha kuubeba msalaba wa wahusika wengine,”alisema.

“Hili sakata ni mfano wa mbinu zinazotumika kwa kuchukua tatizo la mwingine na kulipandikiza kwa mwingine ili kuficha udhaifu wa wengine. Nadhani imefika wakati Lowassa na yeye aseme wazi, kwa sababu akiacha litaendelea kumuumiza. You need to talk (unahitaji kuongea).”

Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa (UDSM), Richard Mbunda anaona suala hilo halitaweza kuzimika mpaka taarifa nyingine zinazohusiana na kashfa hiyo zitakapoibuliwa.

“Kwa sasa kuna kundi linaloamini kabisa kwamba sakata hilo liliandaliwa kwa ajili ya mtu mmoja kwa sababu taarifa za kamati na Serikali hazikuwa za kutosha. Pia, wanajenga hoja kwamba kwa nini baada ya kujiuzulu suala hilo likaishia pale,” alisema.

“Kwanini  iishie hewani? Mahakama ipo na mtuhumiwa yupo na alishasema yuko tayari  kupelekwa mahakamani. Kwa hiyo utaona kuna jambo kama lilipikwa kwa ajili ya mtu mmoja,” alisema.

Mbunda alisema suala hilo linaweza kuwa mtaji wa kisiasa kama lilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Hata hivyo, Mbunda alisema serikalini wapo wanaoamini kwamba suala hilo liliibuliwa baada ya kubaini hali ya ukiukwaji wa maadili ya umma katika uingiaji wa mkataba huo.