Ripoti: Watoto 394 Tanzania walibakwa kila mwezi kwa miezi 6

Muktasari:

Ripoti hiyo inaonyesha kati ya matukio 6,376 ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoripotiwa mwaka huu, 2,365 yametokana na ubakaji.

Dar es Salaam. Ripoti za matukio ya ubakaji zilizokusanywa kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, zimebaini kuwa watoto 2,365 walibakwa katika kipindi hicho ikiwa ni wastani wa watoto 394 kila mwezi.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya haki za binadamu kwa upande wa Tanzania Bara iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2018.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kati ya matukio 6,376 ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoripotiwa mwaka huu, 2,365 yametokana na ubakaji.

Idadi hiyo imeongezeka maradufu ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwaka uliopita ambako watoto wa kike 759 walibakwa.

Ripoti hiyo imeonyesha pia watoto 533 wamelatiwa katika kipindi hicho cha miezi sita ikilinganishwa na watoto 12 waliolawitiwa miezi sita ya kwanza ya mwaka jana.

Akiwasilisha matokeo ya ripoti hiyo, mtafiti wa LHRC, Fundikira Wazambi alisema katika matukio mengi ukatili huo umefanywa na ndugu wa karibu na majirani, huku watoto walio kwenye hatari zaidi ni wenye umri wa kati ya miaka mitatu hadi 14.

Alisema matokeo hayo ni kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi, ripoti za mashirika, vyombo vya habari na taarifa zinazopokewa na vitengo mbalimbali vya LHRC.

Akizungumzia suala hilo, mwanzilishi wa Jukwaa la Harakati za Masula ya Wanawake wa Kiafrika (AFF), Demere Kitunga alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa kuna tatizo kubwa ndani ya jamii.

Kitunga alisema upo uwezekano wa kuwapo kwa tatizo katika utungaji wa sheria zinazohusu ukatili wa watoto na wanawake.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Vicencia Shule alisema hali hiyo imechangiwa na jamii kutoshiriki kuwalinda watoto hadi wanaangukia kwenye mikono ya watu wabaya. Dk Shule aliitupia lawama Serikali kwa kuweka nguvu katika mambo mengine na kushindwa kuwalinda watoto.

Sanjari na hilo, ripoti hiyo pia imeonyesha kuongezeka kwa ukatili wa kingono na kimwili kwa wanawake na rushwa ya ngono maeneo ya kazi na vyuoni.

Ripoti inaonyesha wastani wa wanawake 203 walibakwa kila mwezi katika kipindi cha Januari hadi Juni. Kwenye ukatili wa kimwili, inaonyesha kuwa wapo wanawake ambao wamepoteza maisha kutokana na vipigo kutoka kwa wenza wao hasa kwa sababu za wivu wa mapenzi.

“Wapo wanawake ambao walipigwa, kuunguzwa moto, kuchomwa na vitu vyenye ncha kali hata kuuwaa kikatili mfano ni yule mwanamke aliyeuawa na mumewe kule Kakonko (mkoani Kigoma) kwa kosa la kuzaa watoto wa kike pekee,” alisema Wazambi.

“Vilevile bado kuna changamoto ya rushwa ya ngono kwenye maeneo ya kazi na vyuoni na ripoti inaonyesha kuwa tatizo kubwa lipo kwenye tasnia ya habari.”

Upande wa haki za kiraia na kisasa, ripoti imeonyesha kupungua kwa matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina kutoka 172 nusu ya kwanza ya mwaka jana hadi 106 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu. Kwa matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi ripoti inaonyesha yameendelea kupungua kutoka 482 ya mwaka jana hadi 395 mwaka huu.