Thursday, January 26, 2017

Wanne wauawa kwa risasi Arusha

Mtoto Isaya Thomas (13) ambaye ni mmoja wa

Mtoto Isaya Thomas (13) ambaye ni mmoja wa majeruhi aliyepigwa risasi baada ya kutokea vurugu baina ya wafugaji na askari wa Suma JKT, wilayani Arumeru mkoani Arusha, akiwa amelazwa kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, jana. Picha na Mussa Juma. 

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Arusha/Serengeti. Watu wanne wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine saba kujeruhiwa katika matukio mawili baada ya kuzuka vurugu wakati askari wa Suma JKT mkoani Arusha na wa Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara walipokuwa wanakamata mifugo ya wafugaji iliyokutwa katika maeneo yanayolindwa.

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha imesema watu wanne walikufa huku watano wakijeruhiwa akiwamo mtoto wa miaka 13 baada ya vurugu kuibuka kati ya wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa na askari wa Suma JKT wanaolinda shamba la miti la Serikali la Meru lililopo wilayani Arumeru.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 11 alasiri katika Kijiji cha Kandaskirieti, Kata ya Oldonyosambu baada ya askari hao kukamata ng’ombe, mbuzi na kondoo na kuanza kuwapeleka kwenye zizi la Serikali kwa maelezo kuwa waliingizwa kulishwa katika msitu wa shamba hilo. Hata hivyo, wafugaji walipinga maelezo hayo.

Aidha, Jeshi la Polisi mkoani Mara limesema watu wawili akiwamo mtoto wa miaka 12 wakazi wawili wa Kijiji cha Njoro Loliondo wilayani Ngorongoro walijeruhiwa mmoja kwa risasi na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti baada ya kuzuka vurugu wakati wa kukamata mifugo iliyokutwa inachungiwa ndani ya hifadhi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo aliwataja waliopoteza maisha kwa kupigwa risasi kuwa ni mfugaji Mbayani Melau (27) mkazi wa Olkokola, Julius Kilusu (45) mkazi wa Oldonyosambu, Lalashe Meibuko (25) mkazi wa Olkokola na Seuri Melita (32) mkazi wa Olkokola.

Kamanda Mkumbo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Isaya Thomas (13) aliyepigwa risasi mgongoni, Mathayo Masharubu (34), Julius Lazaro (32), Evalyn Melio (28) na William Ngirangwa (29) na wote wamelazwa Hospitali ya Mkoa ya Maount Meru.

Kamanda Mkumbo alisema katika operesheni ya kuondoa mifugo ndani ya msitu huo saa 2:30 asubuhi, askari hao walikamata ng’ombe 45, mbuzi na kondoo 65 na kuwapelekea katika zizi la Serikali. Alisema ilipofika saa 11:00 alasiri askari hao walirudi tena kufanya operesheni hiyo na walifanikiwa kukamata ng’ombe 80 na mbuzi na kondoo 70.

“Baada ya kukamata mifugo hiyo, kwa mara ya pili, walikutana na wananchi wakiwa wamebeba silaha za jadi kama mishale, mapanga na fimbo ambao walianza kuwashambulia askari hao kwa lengo la kukomboa mifugo iliyokamatwa,” alieleza Kamanda Mkumbo.

“Baada ya askari hao kuvamiwa walijihami kwa kupiga risasi juu kwa lengo la kuwatawanya lakini hawakutawanyika na waliendelea kuwashambulia askari hao.”

Alisema baada ya kuona mashambulizi yamezidi ndipo askari walipojibu mapigo kwa kuwapiga risasi na watu wanne walifariki dunia na wengine kujeruhiwa. Katika tukio hilo Kamanda Mkumbo alisema hakuna askari aliyeumizwa ila uchunguzi unaendelea kubaini nguvu iliyotumika kwenye mapambano hayo na kwamba askari sita wa JKT wanashikiliwa kwa mahojiano.

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, Jeremiah Onesmo na John Laizer walisema chanzo cha vurugu hizo ni kukamatwa kwa mifugo bila kufuata utaratibu.

Onesmo alisema wamekuwa wakichunga ng’ombe jirani na msitu huo, kwa miaka yote hasa nyakati za kiangazi lakini wanashangazwa juzi kukamatwa mifugo yao na kupigwa risasi ovyo.

Diwani wa Oldonyosambu, Raymond Lairumbe alisema jana kwamba wanapinga kupigwa risasi wananchi hao, kwani tukio hilo lingeweza kumalizwa kwa kufuata taratibu.

“Wananchi walipata hasira baada ya mifugo kukamatwa bila sababu, sasa tukio la kuanza kupigwa risasi ovyo kuwasambaza ndilo limesababisha mauaji. Tunaomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina,” alisema.

Serengeti

Mwandishi wetu ameripoti kuwa watu wawili wakazi wa Kijiji cha Njoro Loliondo walijeruhiwa mmoja kwa risasi na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti baada ya kuzuka vurugu wakati wa kukamata mifugo iliyokutwa ndani ya hifadhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi alisema tukio hilo lilitokea Januari 24 saa nane mchana katika eneo la Mlima Kuka ndani ya hifadhi hiyo, ambako askari wa hifadhi waliokuwa doria walikuta kundi kubwa la mifugo na wakaiweka chini ya ulinzi.

Alisema wafugaji walianza kupiga yowe hivyo kundi kubwa la wananchi likajitokeza na kuanza kuwashambulia askari wa hifadhi waliowazuia kuondoa mifugo hiyo.

Kamanda Ng’anzi aliwataja majeruhi hao kuwa ni Korija Tanin (22) mkazi wa Kijiji cha Njoroi Loliondo ambaye amepigwa risasi mguu wa kulia na Aragali Ngilo (12) ambaye amejeruhiwa baada ya kupigwa wakati wa vurugu hizo na kwamba wamelazwa Hospitali Teule ya Nyerere wilayani Serengeti.

“Wananchi hao walikusanyika kwa wingi katika eneo hilo na kuanza kuwatishia kuwakata na sime askari hao ambao nao katika kujihami walipiga risasi moja ili kuwadhibiti ndipo ilipowapata watu hao waliojeruhiwa,” alisema.

Alisema ameagiza wafugaji hao wafunguliwe jalada la kuingia kwa jinai eneo la hifadhi na askari aliyehusika kupiga risasi naye afunguliwe jalada na uchunguzi ufanyike ili kubaini kama alikuwa sahihi kutumia silaha na kumjeruhi mfugaji huyo.

*Imeandikwa na Anthony Mayunga, Mussa Juma na Zulfa Mussa.

-->