Mkurugenzi wanyamapori kusimamishwa kazi

Muktasari:

Dk Kigwangalla alitoa agizo la kusimamishwa kazi mkurugenzi wanyamapori baada ya kufanya ziara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii Hamisi Kigwangalla ameagiza kusimamishwa kazi Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa kutokana na tuhuma kadhaa, ikiwemo ya kugawa vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria.

Dk Kigwangalla alitoa agizo hilo jana Jumapili Novemba 5,2017 baada ya kufanya ziara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gaudence Milanzi kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo ili kupisha uchunguzi.

Mkurugenzi huyo pia anahusishwa na tuhuma za kuihujumu Serikali kwa kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari zinazochochea mgogoro katika Pori Tengefu la  Loliondo.

Anadaiwa kuvujisha taarifa za msafara wa waziri huyo kwenye mitandao na kusababisha ufuatiliwe na watu wasiojulikana hali inayohatarisha usalama wake.

Pia, anatuhumiwa kwa mambo mengine kadhaa ambayo kwa sasa hatuwezi kuyaandika hadi upande wa pili utakapopatikana.

Dk Kigwangalla ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ili hatua zichukuliwe.

Dk Kigwangalla amesema ili kuimarisha ulinzi wa mpaka wa Mashariki mwa Serengeti, amewaondoa askari wote wa Kituo cha Geti la Kleins.