MAONI: Hongera Mkapa kuweka bayana mazuri, mabaya

Katika uzinduzi wa kitabu chake cha “My Life My Purpose” jana jijini Dar es Salaam, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amezungumza mambo mbalimbali yaliyotokea katika utawala wake, mambo chanya na hasi.

Kati ya mengi aliyozungumza, moja ambalo limeonekana kuvuta hisia za wengi ni kujutia mauaji yaliyotokea Kisiwani Pemba mwaka 2001 na kusababisha vifo vya watu 22.

Mkapa, ambaye alikuwa Davos, Uswisi akihudhuria mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF) wakati mauaji hayo yanatokea, amesema anawajika kwa asilimia mia katika mauaji hayo na anakiri kuwa tukio hilo litaendelea daima kuwa doa katika urais wake licha ya kwamba hakuwepo nchi wakati huo.

Mkapa pia ameeleza hali ambayo polisi walikuwa nayo kabla ya kuamua kufyatua risasi zilizoua watu 22 katika kisiwa cha Pemba ambacho wakati huo kilikuwa kimejaa wafuasi wa CUF.

Ni kitu kikubwa kwamba mtu aliyefikia ngazi ya urais kuamua kuandika kitabu kuhusu maisha yake wakati akiwa Ikulu na kuweka bayana mazuri na mabaya aliyopitia, sababu zilizomfanya achukue maamuzi hayo na kuonyesha kujutia baadhi ya mambo.

Mauaji ya Pemba yanaendelea kukumbukwa kama moja ya matukio ya kihistoria katika anga za siasa yaliyoaacha maisha ya watu wengi yakipotea kutokana na imani yao kwa itikadi fulani. Hivyo, kwa kiongozi kuibuka na kuweka bayana kilichotokea na jinsi alivyoshughulikia ni wazi kuwa anaweza mfano na mwongozo ambao viongozi wa sasa na wa baadaye wanapaswa kufuata.

Hali kadhalika, Mkapa anatumia kitabu hicho kueleza mazingira yaliyosababisha achukue baadhi ya maamuzi ambayo kwa kiasi fulani yaliumiza mamilioni ya Watanzania na mengine kufurahisha mamilioni wengine. Ni kutokana na kuelewa mazingira hayo, gubu lililojengeka rohoni mwa baadhi ya wananchi walioumizwa na maamuzi hayo, linaweza kupungua na hivyo kuondoa roho ya chuki iliyokuwa imejengeka na hivyo kurejesha upendo na amani.

Hatua ya kukiri pia inaelimisha kuwa wote ni binadamu ambao wanaweza kukosea katika kufanya maamuzi akiwa kiongozi na baadaye kurudi katika jamii ile. Hivyo, kujutia makosa ni kitu kikubwa kwa binadamu yeyote kama anataka kuishi vyema kwenye jamii yake.

Wakati kauli kama hizo za kujutia kilichotokea zikipunguza gubu miongoni mwa wananchi, maelezo ya jinsi alivyoshughulikia kumaliza tatizo na kutafuta muafaka, yanaweza kuwa somo kubwa kwa viongozi wa sasa na viongozi wa baadaye.

Lazima tujifunze kutokana na makosa yetu na tutafute njia za kusahihisha yale tuliyokosea.

Haya pia yametokea katika nchi nyingine ulimwenguni.

Mwaka 2015, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair aliomba radhi na kukiri kukosea kwa namna nchi yake ilivyoshiriki vita dhidi ya Iraq mwaka 2003.

Mwaka 1987, Rais wa Marekani, Ronaldo Reagan alijutia na kukiri kosa kwa namna ambavyo taifa hilo lilivyoshughulikia migogoro yake na Iran. Hata kiongozi wa kidini, Papa Francis aliomba radhi kwa niaba ya Kanisa Katoliki duniani baada ya ripoti kutangazwa kwa miaka 10 watoto zaidi ya 1,000 wa Pennsylvania wwakilawitiwa na kunajisiwa na mapadri na maburuda.

Mifano ni mingi lakini kilicho wazi ni kwamba Mkapa ametoa somo zuri kwa viongozi wa sasa na wa baadaye.