Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magonjwa mawili yanayoitesa CCM

Muktasari:

  • Katika utekelezaji wa kalenda ya uchaguzi ulioanza Julai mwaka huu, tayari umekamilika kwa zaidi ya asilimia 97 kuanzia mashina hadi majimbo unaohusu uongozi ndani ya chama huku wilaya nne kati ya 161 zikifutiwa mchakato huo kwa sababu wagombea hawakuwa na sifa na ni watu hatari kwa chama.

Matumizi ya rushwa na makundi ya wasaliti ni ugonjwa unaoendelea kujitokeza ndani ya Chama cha Mapinduzi(CCM),licha ya vita iliyotangazwa na mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais John Magufuli kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.

Katika utekelezaji wa kalenda ya uchaguzi ulioanza Julai mwaka huu, tayari umekamilika kwa zaidi ya asilimia 97 kuanzia mashina hadi majimbo unaohusu uongozi ndani ya chama huku wilaya nne kati ya 161 zikifutiwa mchakato huo kwa sababu wagombea hawakuwa na sifa na ni watu hatari kwa chama.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey anasema chama hakitasita kuchukua hatua dhidi ya kiashiria chochote cha rushwa kwa wagombea.

Uchaguzi huo unaogusa idadi ya wanachama wake hai milioni nane nchini kama ilivyoelezwa na mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete, pia umeshafanyika katika Jumuiya zake zote karibu asilimia mia moja hadi ngazi ya majimbo.

Vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), vilivyofanyika siku nne zilizopita chini ya Rais Magufuli, vilijadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama wanaoomba uongozi ngazi za wilaya.

Hata hivyo, changamoto mbili zimeendelea kukitesa chama hicho kila inapoingia katika vipindi vya chaguzi za ndani, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Changamoto ya kwanza ni mwendelezo wa viashiria vya rushwa kupitia wagombea ngazi mbalimbali huku Polepole akitoa onyo kali dhidi ya wale watakaobainika kwamba, watafukuzwa uanachama na kufuta uchaguzi pia.

Ugonjwa wa pili unahusisha kundi la watu hatari lililosababisha kufutwa kwa mchakato wa uchaguzi katika wilaya hizo. Hali hii ni mwendelezo pia wa wimbi la usaliti kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ugonjwa wa rushwa

Kuhusu vita ya rushwa, Polepole anasema Chama hakitasita kufuta uchaguzi na kumfuta uanachama mgombea atakayebainika kuwa kinyume na taratibu za chama ikiwamo matumizi ya rushwa.

Polepole anasema lengo la mabadiliko ndani ya chama hicho ni kuifanya CCM mpya kwa kuwapata viongozi wasafi na waaminifu ndani ya chama na kuendana na kasi ya rais John Magufuli.

Hata hivyo, vita hiyo inaonekana kufifia nje ya chama hicho baada ya wabunge wawili wa Chadema Godbless Lema na Joshua Nassari kuibua tuhuma za rushwa huku wakiweka wazi ushahidi unaohusisha njama za CCM kutumia rushwa katika wimbi la madiwani wanaotoka Chadema kujiunga CCM.

Nassari anasema madiwani hao waliofikia kumi kutoka halmashauri tatu za Mkoani Arusha, walikuwa wakiahidiwa fedha, ajira na kukamilishiwa miradi ya maendeleo katika kata zao, kulipwa kiinua mgongo cha miaka yote mitano kati nafasi zao.

Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anasema vita ya rushwa haina mipaka katika vita yake na CCM haina budi kushughulikia udhaifu utakaojitokeza katika tuhuma za rushwa kwa wanachama wake ngazi ya halmashauri tatu za mkoa wa Arusha.

Profesa Shumbusho anasema vita hiyo ndani ya CCM itafsiri uhalisia katika vita hiyo kwa Watanzania bila kujali masilahi yake kisiasa. “Haingii akilini kwa mwenyekiti aliyejipambanua kupambana na rushwa harafu akaliacha suala hili, anatakiwa kuishughulikia dosari hiyo kwa wahusika wote watakaobainika,”anasema.

Anasema endapo CCM haitachukua hatua kali dhidi ya tuhuma hizo za rushwa kwa madiwani, itapunguza ushawishi wake katika vita inayoendesha ndani ya uchaguzi unaoendelea kwa sasa. “Watanzania wataona kumbe CCM inafanya mzaha tu na vita ya rushwa inayofanyika itaonekana kuwaonea watu tu,kwa hiyo lazima ccm itafakari hilo,”anasema.

Polepole anasema tuhuma hizo hazina mashiko kwani madiwani hao wanayo haki ya msingi ya kuamua na wanavutiwa na kasi ya rais John Magufuli, akikejeli udhaifu kwa madiwani wao kupokea rushwa endapo tuhuma hizo ni kweli.

Ugonjwa wa wasaliti

Katika ugonjwa mwingine ulioathiri uchaguzi huo mwaka huu ni pamoja na Chama hicho kubatilisha chaguzi katika kata 44 kutokana na kubainika mambo yaliyopigwa marufuku kama vile makundi, kupanga safu na kuweka mapandikizi au wasaliti.

Mambo mengine yaliyojitokeza ni kupitisha wagombea ambao ni watuhumiwa wa ubadhirifu wa mali za chama; wasio wakazi wa maeneo husika; waliopitishwa baada ya wengine kuonewa katika uteuzi, kuwapo mgombea mmoja tu aliyepitishwa na kutolewa taarifa kuhusu wagombea zenye lengo la kupotosha vikao vya juu.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Kigoma, Dk Amani Kaborou aliliambia gazeti hili kwamba, ndani ya chama hicho kuna watu ambao hawajaukubali mfumo huo mpya wa uchaguzi.

Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakipanga safu kwa kutoa fomu kwa watu wanaotaka wagombee au kuwanunulia kadi za uanachama ili baadaye waweze kuwachagua na wengine huficha fomu na kuwapa wagombea wao.

“Matatizo tunayokumbana nayo katika uchaguzi yanaweza kusemekana yanaanzia na uchaguzi huu, kwa kuwa umekataza kabisa kabisa kupanga safu, yaani kuteua watu ambao baadaye watakuja kukupigia kura wewe katika awamu yako,” alisema Dk Kabourou.

“Hilo la safu kwa kweli naona watu wengi walikuwa hawajaliafiki. Naona hilo limekuwa kila mahali tangu ngazi ya tawi na kata.”

Magonjwa hayakuanza leo

Vita ya magonjwa hayo ya usaliti na matumizi ya rushwa ilichafua hali ya hewa ndani ya chama hicho mwaka 2011 baada ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete kutangaza mkakati wa ‘kujivua gamba’ akiwataka makada wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari na kujiondoa ndani ya siku 90. Hata hivyo hata baada ya muda huo kumalizika, mkakati huo uliyeyuka na viongozi wakaanza kubadili maudhui yake.

Desemba mwaka 2014, ugonjwa wa wasaliti na rushwa ulikitesa chama hicho wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na viongozi wengine walikuwa mstari wa mbele kukemea udhaifu huo.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye ni kada wa Chadema kwa sasa alijitabiria kukihama chama hicho iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM ingeendelea kulalia kwenye rushwa, huku akionya tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Richard Mbunda anasema changamoto iliyopo katika vita ya wasaliti na rushwa inaathiriwa na mabadiliko ya chama hicho kwa kuwa wastani wa asilimia 90 ya wanachama wake bado wameathiriwa na utamaduni uliomaliza muda wake. “Kwa mfano kuna wanachama ambao ninaamini walikuwa wameweka kwa muda mrefu katika nafasi hizo za uongozi bila kujua hali itakuwaje hapo baadaye kwa hivyo inakuwa vigumu kukubaliana na mabadiliko hayo katika mchakato wa kupatikana viongozi,”anasema Mbunda.

Anasema uzoefu unaonyesha rushwa inatendeka zaidi kwa wanachama wanaowania ngazi za juu ikilinganishwa na ngazi za mashina, matawi na kata.

Mbunda anasema lengo ni zuri katika vita hiyo kwa kuwa ndiyo njia sahihi itakayosaidia upatikanaji wa viongozi wazuri,akisisita rais ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho kusimamia mabadiliko hayo bila kumwonea mwanachama yeyote.

Kuhusu kundi la watu hatari wakiwamo wasaliti, Mbunda anatoa tahadhari kwa chama hicho katika kushughulikia kundi la wanachama hao.

“Wapo wasaliti wa kudumu na wale wanaojitokeza wakati wa chaguzi tu kwenye makundi,inahitaji umakini kuwaadhibu wote kwa pamoja kwa hiyo hao wanaojitokeza kwenye uchaguzi huu ni vyema uongozi ukajiridhisha zaidi,”anasema.

staili mpya ni ugonjwa?

Uchaguzi huo umekamilika ukihusisha Jumuiya ya Wazazi Tanzania, Jumuia za Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), UVCCM kuanzia ngazi ya tawi hadi Jimbo.

Katika uchaguzi unaofanyika kwa utekelezaji wa kalenda ya mwaka 2017, CCM ilieleza katika baadhi ya maeneo uchaguzi huo, yalikumbwa na vitendo visivyofaa na baadhi yake kufutwa na kuagizwa kurudiwa upya.

Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, katika hatua hizo za awali, tayari mashina 220,801 kati ya 222,126 yamekamilisha uchaguzi, pia matawi 22,447 kati ya 23,246 pamoja na kata 3,726 zimeshapata viongozi wake.

Kwa mujibu wa CCM, mabadiliko katika chaguzi ndani ya chama hicho yanamtaka mgombea yeyote aliyeteuliwa kuanzia ngazi za mashina, matawi na kata hadi wilaya kwenda mbele ya wapigakura na kukutana nao kwa mara ya kwanza siku ya uchaguzi badala ya tamaduni uliozoeleka wa kujitangaza kwa kufanya kampeni.

Baadhi ya wachambuzi wa duru za kisiasa wanasema staili hiyo ya uchaguzi inaweza kuwaangusha wagombea wengi au kubatilisha chaguzi kwa watakaokwenda kwa mazoea ya miaka mingi ya kutegemea fedha na umaarufu kama mtaji wao.