Simba, Yanga zaanika faida 3 mabadiliko CAF

Saturday July 20 2019

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mfumo mpya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho kuchezwa mara moja imepokewa kwa mtizamo chanya na viongozi na makocha wa timu ambazo zitaiwakilisha nchi kimataifa.

Kamati ya utendaji cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Juzi katika kikao chake kilichofanyika Cairo, Misri ilifuta mfumo wa mechi za Fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kuchezwa mara mbili nyumbani na ugenini.

Rais CAF, Ahmad Ahmad alisema uamuzi huo umetokana na kutokea kwa vurugu msimu uliopita katika mchezo wa Fainali wa Ligi ya Mabingwa.

Msimu uliopita mechi ya fainali kati ya Esperance ya Tunisia na Wydad Casablanca iliibua vurugu huku Wydad wakigomea kuendelea na mchezo huo wakipinga uamuzi wa refarii, Bakary Gassama wa Gambia kukataa bao lao la kusawazisha.

Juzi CAF imetangaza kuanzia msimu ujao, fainali itakuwa ni moja na itachezwa kwenye uwanja utakaotangazwa na shirikisho hilo.

Mfumo huo wa CAF umepokewa kwa mtazamo chanya na viongozi na makocha wa timu za Simba na Yanga ambazo zitaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa sanjari na wale wa Azam na KMC ambao watashiriki kwenye Shirikisho.

Advertisement

Viongozi hao wametaja faida za mfumo huo mpya ambao wamesema utaondoa urasimu katika kupanga matokeo kwenye mechi za nyumbani, itapunguza migogoro kwa timu kuona kama zinahujumiwa na pia itasaidia bingwa kupatikana kihalali.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema mfumo huo utasaidia kupunguza malalamiko.

“Soka lina mambo mengi, hivyo CAF kuamua fainali iwe moja tena inachezwa kwenye uwanja ambao wao watautaja, itasaidia kwanza timu kujiandaa kweli kweli bila kutegemea njia za mkato kupata matokeo,” alisema Mwakalebela.

Mlezi wa timu ya KMC na Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta alisema mfumo huo wa CAF utasaidia kuondoa mtizamo wa kutegemea ushindi wa nyumbani.

“Kutakuwa kuna vitu vingi wameangalia, lakini hii sasa itaondoa mitazamo ya timu kutegemea ushindi wa nyumbani,” alisema Sitta.

Kocha wa Azam, Etienne Ndayiragije alisema uamuzi huo wa CAF utasaidia pia kupunguza malalamiko ya timu inapokwenda kucheza ugenini.

“Hapo kila mtu ‘anakufa’ kivyake, hakuna kusema umefanyiwa hujuma ugenini, mfumo huo kwa kiasi fulani utapunguza malalamiko ya mechi za ugenini hata kwenye ushindani uta-balance,” alisema kocha huyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema CAF imefanya uamuzi sahihi japo wasiwasi ni mashabiki wa timu zote mbili wataweza kusafiri kwa wingi kwenda kushuhudia fainali ya timu hizo kwenye uwanja wa ugenini?

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema utaratibu wa uwanja wa nyumbani ulikuwa na tafsiri tofauti Afrika.

“Wenzetu ukienda kucheza ugenini utazomewa na mashabiki, lakini huduma zingine zote uwanjani zitakuwa fair,” alisema Mayay.

Alisema kila uamuzi una faida na hasara ambapo kwenye hili, ile ladha ya ushabiki itakosekana kwani huenda viwanja vikawa vitupu kwenye fainali.

Advertisement