Tanzania mguu sawa tenisi Afrika

Dar es Salaam. Wakati timu ya wasichana chini ya miaka 16 ikitwaa medali ya shaba, wavulana wanahitaji ushindi leo dhidi ya Shelisheli ili kupata medali ya fedha kwenye mashindano ya tenisi Afrika Mashariki na Kati.

Tanzania inahitaji ushindi katika mchezo huo wa tamati ya mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku tisa kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam ili kujihakikishia medali ya pili ya fedha huku Rwanda au Burundi itakayoshinda itapata dhahabu.

Katika mechi hizo zinazochezwa kwa mtindo wa ligi, matokeo dhidi ya Shelisheli yataamua ushindi wa Tanzania ambayo ni ya tatu ikiongozwa na Rwanda, Burundi ambazo zitakutana leo.

Tanzania itashuka uwanjani huku ikiombea Rwanda iifunge Burundi, matokeo ambayo yataipunguza kasi Burundi na kuiwezesha Tanzania kutwaa medali ya fedha endapo itaifunga Shelisheli na Burundi itashushwa hadi nafasi ya tatu.

Rwanda inaongoza kwa pointi tatu sawa na Burundi baada ya kushinda michezo tisa ingawa imeshinda mechi nane na kufungwa moja. Tanzania ya tatu ikiwa na pointi mbili, ikifungwa mechi tano na kushinda nne huku Shelisheli ikishika mkia. Mchezaji Kanuti Alagwa alisema wanafahamu ugumu wa mechi hiyo na umuhimu wa kutwaa medali, hivyo hawataidharau Shelisheli ingawa inashika mkia.

Kanuti aliyetwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya mkondo wa kwanza alisema watapambana ili kubakiza ubingwa nchini.

Katika mechi za mapema za vijana chini ya miaka 14 zilizochezwa jana, Nasha Singo alishindwa kutamba mbele ya Rona Tuyishime wa Rwanda.

Nasha alipoteza seti 2-0 za 6-1 na 6-1 katika nusu fainali ya kwanza ambayo Rona alifuzu fainali na Faith Urassa wa Kenya.

Faith alimfunga Paula Awino wa Uganda kwa seti 2-0 za 6-2 na 6-1 huku Naitoti Singo akiruhusu kipigo cha seti 2-0 za 6-2 na 6-2 dhidi ya Carine Nishimwe.

Naye Rashid Ramadhani na Isaka Ndossi walipoteza mechi zao dhidi ya Emmanuel Manishimwe na Junior Hakizumwamwi wa Rwanda.

Ndossi alifungwa na Manishimwe seti 3-1 za 6-4, 6-2 kwa 6-0. Rashid alipoteza kwa seti 2-0 za 6-0 na 6-0. Mabingwa wataiwakilisha Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya Afrika ya vijana yatakayofanyika baadaye Machi nchini Togo na Madagascar.