Masinga atia simanzi Afrika

Muktasari:

  • Wadau wa soka Afrika, wameeleza kushitushwa na kifo cha aliyekuwa mshambuliaji nyota wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Philemon Masinga.

Johannesburg, Afrika Kusini. Kifo cha mshambuliaji nyota wa zamani wa Afrika Kusini, Philemon Masinga, kimeacha simanzi kwa mashabiki wa soka.

Masinga aliyeng’ara Leeds United iliyokuwa Ligi Kuu England, alifariki dunia juzi akiwa na miaka 49 baada ya kuugua maradhi ya saratani.

Nguli huyo aliyecheza Ligi Kuu England kwa miaka miwili, alikuwa nembo ya Afrika Kusini kutokana na kipaji chake cha kufunga mabao.

Muda mfupi baada ya tangazo la kifo hicho, wadau wa soka waliandika ujumbe wa simanzi kupitia mitandao ya kijamii wakieleza kuguswa na tukio hilo.

Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA), lilisema Masinga alibainika na kansa mwezi uliopita, baada ya kuhamishiwa hospitali ya Johannesburg akitokea nyumbani kwao katika mji wa Klerksdorp.

Wadau wa soka Afrika wamemtaja Masinga shujaa wa Afrika Kusini na atakumbukwa kwa mchango mkubwa aliotoa enzi za uhai wake.

Masinga amecheza katika klabu mbalimbali akianzia na Jomo Cosmos, Mamelod Sundowns, Leeds United, St Gallen, Salernitana, Bari na Al-Wahda.

Nguli huyo ameacha rekodi ya kufunga mabao 154 katika mechi 328 za ligi mbalimbali. Pia amefunga mabao 18 katika michezo 58 ya timu ya Taifa.