Buriani Mzee Akilimali wa Yanga, Kuzikwa kesho Tandale

Muktasari:

Mzee Akilimali atakumbukwa kutokana na misimamo yake dhidi ya viongozi wa Yanga hususan wakati wa uongozi wa Yusuf Manji.

Mwanachama mkongwe wa klabu ya Yanga Ibrahim Omary Akilimali amefariki dunia leo asubuhi ya Desemba 14, katika Hosptali ya Bagamoyo baada ya kuugua Kwa muda mrefu.

“Nimepokea simu leo asubuhi kutoka kwa ndugu wa Mzee Akilimali akinijulisha kuhusu msiba huo. Alisema atanipa taarifa zaidi baada ya kufika Bagamoyo,” amesema Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli.

Akizungumzia msiba huo, Mwenyekiti Umoja wa Tawi la Yanga kwa Mtogole, Waziri Ramadhani amesema marehemu Akilimali ambaye aliwahi kuwa katibu wa Baraza la Wazee Yanga, atazikwa kesho saa 10 katika Makaburi ya Tandale kwa Mtogole.

Mara baada ya taarifa za msiba wa Mzee Akilimali ambaye alikuwa mwanachama wa Yanga tangu mwaka 1972 na ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na misimamo yake ndani ya klabu hiyo, wadau mbalimbali wa michezo wametuma salamu za rambirambi.

Mmojawapo ni msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara ambaye katika ukurasa wake wa Instagram ameandika, “Tumeondokewa na mwamba katika miamba ya kabumbu nchini. Mzee wetu, baba yetu na mwenyekiti wa Baraza la Wazee Yanga, Ibrahim Akilimali katangulia mbele ya haki. Poleni familia, poleni sana Wanayanga, hakika huu ni msiba wetu sote na tutashiki kikamilifu kwenye majonzi haya.