Cristiano Ronaldo aitwa mzururaji na kuambiwa aondoke Madeira

Cristiano Ronaldo ameitwa “mzururaji” na kuamriwa aondoke katika mji wa Madeira nchini Ureno na mwanasiasa mmoja baada ya picha kuibuka zikimuonyesha nyota huyo wa Juventus akitembea mitaani na familia yake wakati huu wa janga la ugonjwa wa corona.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun ya Uingereza, mwanasiasa huyo, Rafael Macedo, alimshambulia vikali Ronaldo katika mtandao wa kijamii wa Facebook baada ya kuona picha zake akiwa anatembea na mpenzi wake Georgina Rodriguez na watoto wao katika mji huo ambao ndipo mwanasoka huyo alipozaliwa.

“Namtaka mnyama huyo aliyekuja kutoka Italia kukaa nyumbani.  Niondoleeni mzururaji huyo katika mji wa Madeira.”

Lakini katika andiko lingine katika Facebook, Macedo alisema: “Akaunti yangu ilidukuliwa. Siwezi kutoa kauli mbaya kama hiyo dhidi ya CR7 wetu. Hii sio mara jambo kama hili kutokea, na nimeshabadilisha nywila zangu.

“Ninamtaka radhi Ronaldo. Kuanzia sasa nitakuwa nikibadilisha nywila zangu kila wiki. Wadukuaji kuweni makini.  Kuanzia sasa nitakuwa nikifuatilia kwa makini.”

Alisema kwamba atatoa taarifa polisi, na kuongeza: “Siwezi kutumia maneno ya kukera kama hayo. Ninaomba radhi kwa kila mtu, hasa CR7 na familia yake ambao ninawathamini sana, kwa kile kilichotokea.