Dully Sykes, Lady Jay Dee majaji wapya BSS msimu wa 10

Tuesday September 17 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati msimu wa kumi wa kusaka vipaji vya kuimba katika shindano la Bongo Star Search (BSS) ukitarajiwa kuanzia Septemba  28 hadi 29, 2019 mmoja wa majaji maarufu Salama Jabir hatakuwepo kwa mara ya kwanza kama jaji wa shindano hilo tangu lilipoanzishwa miaka 10 iliyopita.

Hatua ya kusaka vipaji itaanza mkoani Arusha, ikifuatiwa na Morogoro, Mwanza, Mbeya Dodoma na kumalizia  Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Septemba 17, 2019 na  Mkurugenzi wa BSS, Ritha Paulsen kwenye mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesema msimu huu kutakuwa na sura mpya za majaji.

Amewataja majaji hao kuwa ni Lady Jay Dee na Dully Sykes huku wa zamani akibaki yeye kama jaji mkuu na Master Jay ambaye wamekuwa naye kwa kipindi chote.

“Salama amebanwa na shughuli nyingi, ndiyo maana kwa mara ya kwanza hatakuwa kama jaji kwenye shindano hili, ”amefafanua Ritha.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa jaji wa shindano hilo ka mara ya kwanza mwimbaji wa Bongofleva Dully Sykes amesema  amefurahi kuaminiwa kuwa kati ya majaji katika shindano hilo.

Advertisement

“Nina uzoefu wa miaka 20 katika soko la muziki ambapo waandaaji wameamini nitawachaguliwa mshindi anayestahili,” amesema.

Kwa upande wake, Lady Jay Dee amesema anashukuru kwa mara ingine kufanya kazi na Master Jay ambaye alikuwa ndiye aliyemtengenezea albamu yake ya kwanza ya 'machozi'.

“Ninarudi kufanya kazi na watu nilioanza nao muziki, kutafuta vipaji vipya vya tasnia hiyo, nakumbuka Master Jay alitengeneza albamu ya machozi, huku  Benchmark ndio kampuni iliyopiga picha za video za albamu hiyo.”

“Kuna wasanii walikuwa wanatamani kufanya kazi na mimi, kupitia BSS watapata jukwaa la kufanya hivyo,” amesema Lady Jay Dee.

Shindano hilo lililodhaminiwa na kampuni ya king'amuzi cha Startime na Tume ya kupambana na kudhibiti Ukimwi (Tacaids)  litakuwa likionyeshwa katika Chanel ya StarSwahili.

Advertisement