Kocha Eymael apambana na mwamuzi Uwanja Uhuru

Muktasari:

  • Eymael ambaye anaiongoza Yanga kwa mara ya kwanza alionekana muda wote akitoa maelekezo kwa wachezaji wake na mara kadhaa alionekana kumlalamikia mwamuzi wa mezani wakati mechi ikiendelea.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael ameanza kibarua chake kwa kupambana na mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu wakati timu yake ikipokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mabao ya Yusuph Mhilu, Ally Ramadhan na Peter Mwalianzi yameipa Kagera Sugar pointi tatu na ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Yanga.

Yanga ikicheza pungufu baada ya kiungo wake, Mohammed Issa ‘Banka’ kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano, hali iliyomfanya kocha Eymael kupoteza utulivu katika benchi lake tangu mwanzo wa mchezo hadi mwisho.

Mbali na kipigo hicho, kocha wake mpya Eymael alijikuta akiingia uwanjani kumfuata mwamuzi, Mwinyimkuu na kuonekana kuzoza mara baada ya filimbi ya mapumziko.

Tukio hilo lilifanya kocha huyo kuibua maswali kwa mashabiki waliojitokeza kwa uwanjani hapo.

Eymael ambaye anaiongoza Yanga kwa mara ya kwanza alionekana muda wote akitoa maelekezo kwa wachezaji wake na mara kadhaa alionekana kumlalamikia mwamuzi wa mezani wakati mechi ikiendelea.

Kocha huyo alionekana kuwa na jazba ya kuzunguka nje ya korido la ukumbi wa mikutano wakati mwenzake wa Mtibwa akizungumza na Wanahabari alionekana kumfokea mwamuzi, Mwinyimkuu na kumlalamikia yule wa mezani, Elly Sassi mara kadhaa.

Akizungumzia kipigo hicho, Eymael alisema yametokana na makosa ya mabeki aliodai walifanya makosa matatu yaliyowagharimu.

Kocha huyo alisema mabeki walishindwa kujipanga vyema hatua iliyotoa nafasi kwa Kagera kuliandama lango lao mara kwa mara.

“Ni makosa ya kiufundi yaliyofanywa na mabeki, walitoa mwanya kwa Kagera, si kwamba walicheza vibaya, walifanya makosa matatu ambayo yametugharimu,”alisema Eymael.

Mabeki wa kati Kelvin Yondani na Lamine Moro walicheza kwa kutoelewana hatua iliyotoa nafasi kwa Yusuph Mhilu na Kelvin Sabato kuwapenya mara kwa mara.

Yondani na Lamine walifanya makosa ya mara kwa mara ambayo yalimuweka katika mazingira magumu kipa Farouk Shikalo.

Mhilu ambaye amewahi kucheza Yanga kabla ya kutemwa, aliwatoka mabeki hao ambao walishindwa kumdhibiti.

Pia alisema Yanga ilikuwa na nafasi nzuri ya kufunga idadi kubwa ya mabao, lakini washambuliaji wake walikosa umakini walipoingia ndani ya eneo la hatari la Kagera.

Alisema tangu makosa ya safu ya ulinzi na ushambuliaji alianza kuyabaini mapema katika mazoezi, lakini ataendelea kuyafanyia kazi.

“Si kwamba Kagera ni timu bora sana kuliko Yanga, walipata nafasi wakazitumia,”aliseka kocha huyo ambaye wakati wa mapumziko alimsogelea mwamuzi wa mchezo huo timu zilipokuwa zikienda vyumbani.

Awali, Eymael alisema haifahamu Kagera lakini amejipanga kupata ushindi kwa kuwa amepata taarifa zao kupitia kwa wasaidizi wake.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo alipoanza kuinoa timu hiyo kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Dar es Salaam.

Wakati Eymael akitoa sababu za kipigo, kocha wa Kagera Mecky Maxime alisema wametumia udhaifu wa Yanga katika eneo la ulinzi kufunga mabao hayo.

Maxime alisema baada ya kupoteza mechi tatu zilizopita, walijipanga kushinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Safu ya kiungo ya Yanga ilipwaya na kufanya idadi kubwa ya wachezaji wa Kagera kumiliki mpira kwa muda mrefu sanjari na kutengeneza mashambulizi mengi.