Metacha aibeba Yanga ikilazimisha suluhu kwa Coastal Union Uwanja Mkwakwani

Sunday February 23 2020

 

By Burhan Yakub

Tanga. Yanga imeendelea kujitoa katika mbio za ubingwa wakipata sare ya nne mfululizo baada ya kukubali kulazimisha suluhu na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kubaki nafasi ya nne ikiwa na pointi 41, Coastal Union imebaki nafasi ya tano na pointi 39, wakati Simba ikiongoza ligi kwa pointi 62, ikifuatiwa na Azam (45) na Namungo (43).
Katika mchezo huo makipa Soud Abdallah wa Coastal Union na mwenzake Mechata Mnata wa Yanga wameonyesha kiwango cha juu na kuzifanya timu hizo kutoka suluhu.
Katika mchezo huo uliokuwa na upinzani kipa wa Coastal Union, Abdallah alifanya kazi nzuri kuokoa hatari za washambuliaji wa Yanga katika dakika zote walizokuwa wakishambuliwa.
Kipa Abdallah aliokoa mpira wa juu uliopigwa na Benard Morrison pia aliokoa mashambulizi ya washambulia Tariq Seif na Ditram Nchimbi.
Yanga watajilaumu wenyewe kwa kutawala mchezo katika kipindi cha kwanza pamoja na kupata kona tisa (9) na kushindwa kuzitumia huku wenyeji Coastal wakipata kona moja.
Katika kipindi cha pili Coastal Union ilibadilika na kuwa bora zaidi kwa kulishambulia mara kwa mara lango la Yanga walionekana kuchoka.
Kipa Mechata wa Yanga alifanya kazi nzuri kumzuia mashuti ya Ayoub Lyanga, Ugando na kuinusuru timu yake isipate kipigo.
Baada ya filimbi ya mwisho Jeshi la Polisi walilazimika kutuliza ghasia kutokana na mashabiki wa Yanga kumng'ang'ania shabiki Coastal Union akidai amewaibia simu jambo lililosababisha kundi la mashabiki wa Coastal Union kuvamia upande wa Yanga.
Katika mchezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa leo Jumapili; Tanzania Prisons ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma imepata ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi Lipuli.
Mshambuliaji Salum Kimenya alifunga bao la kwanza Prisons katika dakika 12, kabla ya Ismail Aziz kupachika bao la pili katika dakika 90.
Ushindi huo unaifanya Prisons kufikisha pointi 33 na kupanda hadi nafasi ya tisa (9) katika msimamo wakati Lipuli imebaki katika nafasi 12.
Mwanza, Alliance FC ikiwa nyumbani imelalazimishwa sare ya bao 1-1 na Singida United kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Wenyeji Alliance FC walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika 10, kupitia Sameer Vicent kabla ya Singida United kusawazisha bao hili dakika 53 kupitia Stephen Kwame.

Advertisement