Nyota wa Madrid hatarini kufungwa miezi sita

Friday October 23 2020
madrid pic

Belgrade, Serbia . Mshambuliaji wa Real Madrid, Luka Jovic anaweza kukumbwa na hukumu ya miezi sita jela nchini Serbia kutokana na tuhuma za kukiuka masharti ya karantini, waendesha mashtaka wa serikali wamesema leo Ijumaa.

Mwezi Machi, klabu hiyo ya Hispania ilimruhusu Jovic kuondoka ili akatulie na familia yake, lakini vyombo vya habari vya Serbia viliripoti kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alionekana akikata mitaa ya Belgrade na kupata kinywaji pamoja na wanasoka wenzake.

Waendesha mashtaka wa Serbia wanaiomba mahakama itoe hukumu kwa kosa la kuondoka "sehemu ya makazi" licha ya kwamba alitoka katika "nchi iliyokuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona".

Chini ya kanuni za wakati huo, alitakiwa ajitenge kwa wiki mbili.

Waendesha mashtaka wanalipeleka shauri la Jovic mahakamani baada ya mshambuliaji huyo kukataa kulipa dola 35,556 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh 70 milioni za Kitanzania) kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, kiwango ambacho walipendekeza kuwa fidia ili mashtaka yake yafutwe.

Wakati huo, waziri mkuu wa Serbia, Ana Brnabic aliwashutumu "wanasoka wanaotoka nje" kwa kuonyesha mfano mbaya, wakati nchi hiyo ikiwa katika wiki ya kwanza ya kutangaza dharura baada ya mlipuko wa corona.

Advertisement

 

Advertisement