Shabiki wa Algeria agonga familia, aua

Duka la pikipiki likiwa limevugika baada ya watu kuvamia na kuiba vifaa wakati mashabiki wakishangilia ushindi wa Algeria dhidi ya Ivory Coast jana. AFP

Muktasari:

  • Shabiki huyo anayeishi Marseille nchini Ufaransa alikuwa akiendesha gari kwa kasi baada ya Algeria kuishinda Ivory Coast kwa penati katika mechi ya fainali za Mataifa ya Afrika zinazoendelea nchini Misri.

Marseille, Ufaransa. Shabiki wa soka wa Algeria aliyekuwa akishangilia ushindi wa timu yake jana, alishindwa kulimudu gari na kugonga familia moja kusini mwa Ufaransa usiku wa kuamkia leo, ajali iliyosababisha mwanamke mmoja kuuawa na mtoto wake kuumia vibaya, maofisa wa usalama wamesema.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 21 alikuwa akiendesha gari lake kwa mwendo wa kasi katika maeneo ya Mosson katika jiji lililo kusini la Montpellier jana usiku, alisema ofisa wa usalama akiongeza kuwa dereva huyo alipelekwa mahabusu.
Mwanamke aliyegongwa alikuwa akitembea na mtoto wake wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja wakati ajali hiyo ilipotokea.
Mtoto huyo alipata majeraha na kupelekwa hospitali, alisema ofisa huyo.
"Kwa sasa tunajaribu kutathmini mazingira ya tukio hilo," alisema na kuongeza kuwa "kuliku ana watu wengi mitaani" baada ya ushindi huo wa Algeria dhidi ya Ivory Coast katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).
Katika tukio jingine, maduka mawili yaliyo karibu na Champs-Elysees jijini Paris yalivamiwa usiku wa kuamkia leo Ijumaa wakati mashabiki wakishangilia ushindi huo.
Maelfu ya watu walikusanyika katika eneo hilo kushangilia ushindi huo ambao umeipeleka Algeria nusu fainali ya Mataifa ya Afrika.
Lakini wakati mashabiki wakishangilia ushindi, kundi la watu lilivamia maduka yaliyokuwa karibu, likiwemo la vifaa vya pikipiki, mwandishi wa AFP alisema.
Watu kadhaa waliingia kwenye maduka hayo na kuchukua kofia ngumu (helmet), glovu na pia pikipiki, alisema mwandishi huyo.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na angalau mtu mmoja alikamatwa.
Mashabiki wa soka wana utamaduni wa kukutana katika bustani ya Champs-Elysees kushangilia ushindi wa timu zao.