VUNJA MBAVU: Umri sahihi wa wachezaji wetu na hawa Bongo Movie

Sunday November 24 2019

 

By Dk Levy

Tuanze na Samatta. Ni vile tu jamaa anahangaikia maisha. Zaidi anawakilisha nchi ndo maana tumeamua kukausha. Lakini ukweli jamaa ana miaka 34 na ushee. Waliocheza naye utotoni chandimu, hivi sasa wana miaka saba makazini. Ni maofisa wakubwa tu.

Sasa piga hesabu tangu shule ya msingi, sekondari mpaka chuoni. Halafu weka miaka kama mitano ya kuhangaika na bahasha za kaki kusaka ajira. Jasho likiwatiririka bila kupata ajira. Ndo vile sisi tumeamua tukaushe maana tukisema hakuna jipya zaidi ya kumharibia. Ila jamaa ana 34. Kama unabisha utakuwa mchawi. 

Kuna Okwi. Huyu sasa ndo bingwa la kamba. Jamaa alisajiliwa Sport Club Villa ya Uganda 2004. Wakati huo alidanganya ana miaka 22. Ina maana alikuwa na zaidi ya hiyo. Alikuwa na ndoto za kucheza Ulaya. Aliposhindwa akaja Simba 2011 akaongopa ana miaka 19. Tukashangaa kipaji kile kuja Bongo. 

2004 akaenda Yanga. Huko  akawaongopea Gongo wazi ana miaka 26. Wakati kwa umri wa miaka 19 mwaka 2011 ilikuwa awe na miaka 22. Ukiwa muongo uwe na kumbukumbu. Akaondoka na katua tena kwa wauza vijora wa Msimbazi. Akasema ana miaka 27 yaani tangu 2014 mpaka 2016 aliongezeka mwaka mmoja tu. 

Kagere yeye aliacha kabisa kutaja umri. Maana mwili na miaka haviendani. Nasikia kwenye fomu za usajili pale Simba hajajaza sehemu ya umri. Ila kwa mujibu wa wataalamu mlinganisho wa umri na mwili, Kagere ana miaka kama 43 au 44 au 46 kama siyo 41.  Kaseja naye. Kwa kawaida angekuwa ‘stafu’ wa serikalini angekuwa kabakisha miaka michache kustaafu. Kifupi asingemwona rais ajaye akiwa bado anafanya kazi. Sema sasa kwenye ‘pasipoti’ yeye na Elizabeth Michael ‘Lulu’, kiumri wako sawa. Yaani Kaseja ni mdogo hata kwa Mbosso na Lavalava. Kuna Erasto Nyoni bana. Jamaa ukimtazama ni kama ana miaka 28 au 30. Lakini ukweli Karia yule rais wa TFF kiumri ni kama wako sawa. Yaani kwa tabia za Magu za kuteua vijana. Erasto Nyoni asingepata nafasi serikali hii. Yaani jamaa alishasahau ni lini alifikisha miaka 40. Bila mazoezi angekuwa kama Mwalimu Kashasha.

Hawa ni wachezaji wanazuga kwa umri ili watafune pesa. Sasa wameigwa na Bongo Movie na Bongo Fleva. Wema, Wolper na Uwoya wamegoma kuendelea kukua. Wote waliishia kufanya ‘besdidei’ wakiwa na miaka 28. Baada ya hapo wamekausha kabisa. Hata uwavute na greda hawasogei kwenye miaka 30.

Advertisement

Yaani hata uwape pesa wataje miaka halisi watagoma. Nadhani nao wana soka lao la kulipwa la chini ya miaka 30. Sasa hawataki kuonekana wazee. Wengi walipokuwa wadogo walizidisha umri ili waingie maeneo ya wakubwa. Ama kushiriki mashindano ya kikubwa. Sasa wanatamani wawe watoto kila siku. Wamegoma kukua zaidi. 

Nenda popote uliza umri wa Hamisa Mobetto. Tangu mwaka majuzi yeye ana miaka 24. Ukianza kufuatilia elimu yake na matukio aliyofanya kama kuishi na watu na kujifungua. Haviendani na miaka 24. Kuna siku alitueleza amekuwa na Diamond kwa miaka tisa. Usiulize aliishi na Majizo na Mondi kwa pamoja?

Cha kufanya piga hesabu za miaka 24 toa miaka 9 ya kuwa na Mondi. Na hilo alilisema mwaka juzi ambapo Mondi alikuwa hana hata miaka nane kwenye game. Hawa wadada wameamua kuiga kwa kaka zao wa soka. Tusiwalaumu sana. Ni mwendo wa kugandisba umri kama ukwaju wa Bakhressa.

Advertisement