Niyonzima aipeleka Yanga robo fainali Kombe la FA, Azam yapeta

Wednesday February 26 2020

 

By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam.Yanga imeungana na Simba, mabigwa watetezi Azam kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (ASFC) baada ya kuichapa Gwambina kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Yanga pamoja na kuzidiwa kimchezo na Gwambina lakini juhudi binafsi za kiungo Haruna Niyonzima zilisaidia kupata bao pekee katika dakika 45+2 na kuamsha shangwe kwa mashabiki wake.
Niyonzima alifunga bao hilo akiunganisha mpira wa kona wa Juma Abdul ulioshindwa kuokolewa vema na mabeki wa Gwambina na kumkuta Mnyarwanda huyo aliyepiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Ushindi huo unaifanya Yanga kutinga robo fainali pamoja na Simba, Azam, Kagera Sugar, Alliance, Namungo, Sahare All Stars na Ndanda.
Katika mchezo huo Yanga ilianza kulishambulia lango la Gwambina katika dakika ya kwanza tu nusura ipate bao kama si uhodari wa kipa wa Gwambina, Ibrahim Isihaka kupangua krosi iliyopigwa na Juma Abdul huku mshambuliaji wa Yanga, Tariq Seif akiwa karibu.
Gwambina walijibu mapigo dakika ya 13 baada kwa shambulizi zuri na mpira kumkuta nahodha wait Jacob Massawe aliyeachia shuti kali iliyopaa juu ya lango la Yanga.
Katika dakika ya 15, mwamuzi Nasoro Mwinchui wa Pwani alisimamisha mchezo ili kuruhusu kibendera cha kona kilichokuwa upande wa Kaskazini Mashariki mwa uwanja kutengengezwa.
Kibendera hicho kilianguka hivyo beki wa Yanga, Lamine Moro kuhangaika kukiweka mahali pake na kutumia dakika mbili kabla ya mtu mmoja aliyeonekana Kama mlinzi kwenda kumsaidia naye alitumia dakika mbili hivyo mchezo kusimama kwa dakika nne.
Wakati mpira unaelekea mapumziko kona ya Juma Abdul iliokolewa na wachezaji wa Gwambina na mpira kumkuta Niyonzima aliyeachia shuti kali lililotinga moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha pili Gwambina iliendelea kutawala mchezo, lakini wachezaji wake walikosa umakini katika umaliziaji.
Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Yondani aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Sonso pia alitoka Mapinduzi Balama na Tariq Seif na kuingia Mohammed Issa'Banka na Ykpe Gislain.
Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema wamekutana na ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao tofauti na walivyodhani.
"Gwambina ina wachezaji wazuri na walitupa upinzani mkubwa ila tuseme sisi tulikiwa na bahati leo tukapata ushindi.
Kocha wa Gwambina, Novartus Fulgence amesema lengo lake ilikuwa wapate bao kipindi cha kwanza lakini mpango wake ukashindwa.
“Nguvu zao sasa wanaelekeza kwenye ligi daraja la kwanza kuhakikikisha wanabaki kwenye nafasi yao ya juu ili lengo la kupanda Ligi Kuu litimie.
Mbeya: Mabingwa watetezi Azam FC imefufua matumaini yake ya kutetea ubingwa wake baada ya kuifunga Ihefu Fc kwa mikwaju ya penalti 4-5, baada ya kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Sokoine.
Kocha wa Ifehu, Mwaka Mwalwisi alisema wapinzani wao walikuwa bora na wao walikuwa wanacheza kwa tahadhari kutokana na ukubwa wa timu wanayocheza nao.
"Azam ina wachezaji wenye uzefu mkubwa sana kwahiyo tulikuwa tunacheza nao kwa nidhamu na ilitubeba ndani ya dakika 90 licha ya kufungwa kwa penalti," alisema Mwalwisi.
Kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche alisema washambuliaji wake hawakuwa makini katika kumalizia nafasi walizokuwa wanatengeneza.
"Hatukuwa makini katika nafasi ambazo tunatengeneza, lakini pia wapinzani wetu walitupa ugumu kwasababu walikuwa hawatoki nyuma baada ya kujazana," alisema.
Kagera Sugar wakiwa nyumbani Kaitaba wamefanikiwa kusonga mbele kwa mikwaju wa penalti 2-0 dhidi ya KMC baada ya kulazimishwa sare 1-1 katika dakika 90 za mchezo huo.
Wakati huo huo JKT Tanzania wameshindwa kutumia vizuri uwanja wao nyumbani baada ya kuondolewa mashindano kwa mikwaju ya penalti 5-3 dhidi ya Alliance baada ya kutoka sare 1-1 ndani ya dakika 90.

Advertisement