HUYO NDIYE MUNGU; Dimpoz kamtakia 'RIP' king Zillah

Sunday February 17 2019

 

By Luqman Maloto

AMEONDOKA Mfalme wa Salasala, Godzilla. Cheo kilipopanda akaitwa Kingzilla. Bonge la kipaji. Katika ujenzi wa Hip Hop ya Kiswahili, kuna mchango mkubwa wa simenti za Zilla.

Nimesema simenti nimekumbuka Januari 26, mwaka huu, Zilla aliandika ujumbe Twitter ukasambaa kupita kiasi. Kuna watu wakauchukua na kuutumia pasipo kumpa credit Zilla kama ndiye mtunzi halali wa maudhui. Aliandika: “Pale mnapoamua sasa kutulia na kuanza kuyajenga mahusiano yenu. Ghafla Shetani anaiba simenti.” Inachekesha, inafikirisha na inafundisha. Bila shaka unaweza kuwa uliuona ujumbe huu. Basi kwa taarifa yako, aliyeandika kwa mara ya kwanza ni Zilla.

Janki alikuwa na akili sana. Waza aliwaza nini. Hata hivyo ni ukweli kwamba mara nyingi watu huchezeana kwenye uhusiano. Pale mtu anapoamua kutulia aijenge ndoa au penzi lake, anakuta ni “too late”. Hapo ndipo Zilla alisema, Shetani kaiba simenti. Zilla kakatika ghafla. Taarifa za familia zinasema alikuwa anasumbuliwa na tumbo. Yaani tumbo la fasta tu limeondoka na maisha ya Kingzilla. Kijana mdogo ambaye mwaka huu ametimiza miaka 31.

Instagram nikapata msisimko nilipoona Ommy Dimpoz ambaye afya yake inarejea, akimtakia pumziko la amani Kingzilla. Ommy aliandika: “ Inna Lillah Wainna Ilayh Rraj’uun. Rest In Peace Kingzilla.”

Ujumbe wa Ommy unavuta hisia. Hata watu ‘waliocomment’ kwenye post yake walithibitisha. Kuna waliomkumbusha kuwa kuugua si kufa. Yupo aliandika mistari ya wimbo mpya wa Ommy, “Ni Wewe”, alipoimba mawazo yake siku akifa, familia yake na wanaomtegemea.

Comment ya mistari hiyo, Ommy alijibu: “Alhamdulilah.” Naam, anamshukuru Mungu. Zilla aliyekuwa mzima ameondoka. Haimaanishi Ommy hatakufa, ila hapa ni kuonesha kuwa Mungu ana shani yake. Wagonjwa hupona, wazima hufa. Nani anamkumbuka Vengu wa Ze Comedy? Aliyeshirikiana na Masanja Mkandamizaji, Mpoki, Joti, Wakuvwanga na McRegan kuifanya comedy iwe na soko kubwa Tanzania. Mpaka leo yupo. Aliugua hasa. Picha zikasambaa. Sina hakika alipona au bado, lakini Mungu yupo naye.

Advertisement

UNATAKA KUJUA SABABU?

Tupac Shakur katika wimbo “Letter to My Unborn Child”, verse ya pili, kuna mistari anarapa: “I got shot five times, but I’m still breathin’. Living proof there’s a God if you need a reason.” Akimaanisha alipigwa risasi mara tano na bado anapumua, kuishi kunathibitisha uwepo wa Mungu kama unahitaji sababu.

Mwaka 1994, Tupac alipigwa risasi tano lakini alipona. Je, unataka sababu ya Tupac kupona? Akasema uwepo wa Mungu ndiyo sababu. Mwaka 1996 Tupac alipigwa risasi nne na kufariki dunia. Letter to My Unborn Child ulitoka 2001 katika albamu “Until The End of Time”.

Kufa au kuwa hai sababu ni Mungu. Ommy ameugua muda mrefu. Kafanyiwa oparesheni tumboni katika njia ya chakula mata tatu. Ameamka na kuimba tena. Mungu ndiye sababu. Vengu kaumwa miaka na watu wakakata tamaa, ila bado yupo. Mungu ni sababu. Zilla kachomoka ghafla. Ni Mungu tu! Akiamua anakuchukua kama Ngwair na mazingira yenye utata, au mfano wa Kanumba kimasihara tu eti kwa kisa cha ugomvi na mtoto Lulu. Au unaugua na kufa baada ya kuugua muda mrefu kama Sajuki, Banza Stone, Aisha Madinda, Diana Aston Villa, Rukia Bruno, Christopher Alex aliyepiga penalti ya mwisho dhidi ya Zamalek ya Misri na kuipeleka Simba robo fainali Klabu Bingwa Afrika mwaka 2003.

Mungu akitaka anakuchukua kama Papa Wemba, aliyekatikia jukwaani kwenye tamasha la muziki la Femue, Abidjan, Ivory Coast, Aprili 24, 2016. Au anakutwaa ukijiona ni kijana sana mwenye afya njema kama mchezaji wa kimataifa wa Cameroon, Marc-Vivien Foe aliyefariki dunia uwanjani, Juni 26, 2003, bila kuguswa na mtu yeyote, akiwa na miaka 28.

Foe alikuwa na timu yake ya Taifa, Cameroon katika michuano ya Kombe la Mabara. Alicheza dhidi ya Brazil na Uturuki na kushinda, alipumzishwa dhidi ya Marekani maana Cameroon ilikuwa imeshafuzu. Katika mechi ya nusu fainali, Uwanja wa Gerland, Lyon, Cameroon ikicheza dhidi ya Colombia, mnamo dakika ya 72, katikati ya dimba, bila kuwa na mchezaji mwingine karibu, Foe alianguka na kufariki dunia. Ni sawa tu na janki wa Ivory Coast, Cheick Tiote aliyefariki ghafla mazoezini, Beijing, China, Juni 5, 2017.

Ni binadamu na mwisho wake. Anaweza kufia kwenye daladala kama mwanamuziki wa Msondo, Joseph Maina, Februari 17, 2009. Anaweza akafia kufuani mapenzini au katikati ya ibada. Roho inaweza kumtoka akiwa shereheni au msibani. Anakufa anapokuwa kwenye mwendo, anapokaa au anapolala usingizini. Muhimu kukumbuka ni kuwa maisha ya binadamu hayana guarantee. Ni Mungu tu.

TUMUOMBE MSAMAHA ZILLA

Wiki iliyopita, Zilla aliandika Twitter maneno haya: “One thing is RIP Albert Mangwea true talent. My talent is that level. I played my part. Shukurani niliyopata ni kunicompare na watoto... n all work I put I hated music. Niliuchukia. I was like hawa jamaa ni mataahira?”

Hapa kuna hisia za Zilla. Sijajua ni mistari ya wimbo wake au maneno kwenzi aliyoamua kutwiti, lakini yana ukweli sana. Anasema yeye kipaji chake ni daraja la Ngwair. Alifanya kazi yake lakini watu badala ya kutambua thamani yake, wakaanza kumlinganisha na watoto. Hiyo ikamfanya auchukie muziki.

Hatuwezi kutatua tatizo kwa kulikana. Zilla kwa muda mrefu alinyamazishwa na janki Billnass akafanywa mbadala wake. Yeyote mwenye kujua anatambua kuwa Zilla akisema kufananishwa na watoto, anamaanisha Billnass.

Tunahitaji kumwomba msamaha Zilla. Tulimkosea sana. Zilla alithibitisha kipaji chake kwa uwanda mpana mno. Aliijua Hip Hop na aliweza kurap. Kuna wakati aliporap ungedhani 50 Cent ameamua kurap Kiswahili. Kama Ngwair alivyompatia Mase ndivyo Zilla alivyomkopi 50.

Billnass ni mkali sana. Alipaswa kuachwa afanye muziki wake. Kumfanya Zilla kuwa ngazi ya Billnass ilikuwa total disrespect kwa Zilla. Zilla alivunjiwa heshima sana. Alishafanya mengi kuihudumia nchi kupitia muziki. Ameijenga Bongo Fleva kwa sehemu yake.

Zilla wa Nakataa ft Marco Chali, Stay, I Get High, Milele ft Ali Kiba, Hard Work Pays ft Chege, Lakuchumpa ft Joti, Kingzilla ft Marco Chali, Salasala, Thanks God ft Walter Chilambo na madude mengine, au jinsi Zilla alivyombusti Dogo Janja katika chorus ya Mtoto wa Uswazi. Mpaka hapo unaweza vipi kumlinganisha Zilla na Billnass?

Hata kama wangekuwa wanalingana uwezo, bado unaweza vipi kumfanya Billnass kuwa mbadala wa Zilla? Vipaji vingi vinapotea kienyeji kwa tabia hizi. Miaka ya nyuma watu walijaribu kumwona Joslin ni mbadala wa Blue, matokeo yake Joslin kapotea. AliKiba alipoibuka akaonekana ni mbadala wa MB Dog, juzi hapa Nandy alionekana ni mbadala wa Ruby. Kitambo lilifanyika jaribio la kumfanya Prof Jay kuwa mbadala wa Sugu, Juma Nature kwa Inspector Haroun. Ni tabia mbaya. Tuache vipaji ving’are vyenyewe.

Vipaji vipya vikiibuka vipewe nafasi. Muziki unahitaji vipaji vingi. Haitakiwi vikija vipya, vilivyokuwepo tuviweke kwenye dustbin. Zilla aliumia sana kuona amewekwa dustbin wakati bado kijana mdogo na ana kipaji kikubwa cha kuendelea kuuhudumia muziki.

Matokeo yake Zilla akawa mtu wa chicha. Pombe sana ili kujiliwaza na stress za siasa katika muziki. Alivyopotea ikawa umbea tu, eti Zilla kapotezwa na Billnass. Pumzika Zilla, ila tusamehe sana kwa yote. Binadamu hatuna nidhamu ya mzani wa haki. Tutajifanya kuumia sana baada ya kifo chako. Ila ukweli ni huu; wengi tulikupenda!

Advertisement