Ben Pol ataja orodha ya wasanii 15 bora kwake kwenye miondoko ya Bongofleva ikiwa na mwanadada mmoja

Monday November 18 2019

 

By Evagrey Vitalis, Mwananchi

Dar es Salaam. Unaweza ukashangaa na kujiuliza maswali kwa nini imekuwa hivi haijawa vile lakini siku zote unaambiwa mawazo ya mtu mwingine hayawezi kufanana na yako.
Kila mtu  ana kitu chake anachopenda ni kama kwa wala nyama wanavyoshangaa wasiokula lakini hayo ni mapenzi ya mtu binafsi.
Msanii wa Bongofleva nchini Tanzania Bernad Paul maarufu Ben Paul Novemba 18, 2019 ametumia ukurasa wake wa Twitter kutaja  orodha  ya wasanii wake bora 15 wa miaka 10-20 iliyopita hadi sasa.
Orodha hiyo imeibua maswali mengi miongoni mwa wasanii wakihoji kwa nini huyu yumo na yule hayumo.
Wasanii aliowataja Ngwair, Lady Jay Dee, Professor Jay, Dully Sykes, Juma Nature, AY, Fid Q, Mwana FA, Joh Makini, Ben Pol, Diamond, Mr. Blue, Alikiba, G. Nako, na Nikki Mbishi.
Wachangiaji mbalimbali katika mtandao wa Twitter wameonekana kujiuliza maswali mengi ikiwa ni pamoja na kuhoji baadhi ya wasanii wanaofanya vizuri ambao hajawajumuisha katika orodha hiyo.
Maswali mengi yalikuwa ni kwa nini amewaacha wanawake wa muziki huo na kumtaja mmoja ilihali wapo waliofanya vizuri wengi wakiwatolea mfano wasanii Ray C, Vanessa Mdee, Linah Sanga na wengine
Pia walihoji anawaacha vipi wasanii wakali kama   Chid Benz, Sugu, Q Chillah, TID na  Roma.
Lakini mwisho wa siku tunakubali kuwa ni mawazo yake kulingana na vigezo alivyokuwa anapima navyo wasanii kuingia kwenye orodha  yake.

Advertisement