Diamond kupiga shoo tuzo za CAF mbona haistui?

HARMONIZE amesema mbona haimstui? Ngoma mpya imetoka. Watu wanamtahadhirisha kuwa anaweza kurogwa, eti atafeli. Kaipua mzigo wa kuitwa “Hainistui”, ndani yake ndio anaeleza kwamba atakabili yote. Hakuna la kutisha.

Ni kama sasa, kitaa kinapiga mayowe Diamond Platnumz kupiga shoo kali Misri, katika Tuzo za Glo Caf. Sasa kwani inashitua nini yule “smart hustler” wa Tandale kumiliki jukwaa la utoaji tuzo za Shirikisho la Soka Afrika? Mbona haistui?

Yaani ushituke leo? Una wazimu? Januari 2015, Diamond akiwa ndio anaanza kusaka masafa ya kimataifa, alikuwa miongoni mwa wakali waliofanya kweli kweli Glo Caf Awards 2014. Miaka mitano iliyopita mwanangu.

Au enzi hizo ulikuwa hujatua mjini? Ngoja tuliokuwepo tukusimulie. Mwaka 2014, Diamond alifanya ngoma iliyompeleka mbali sana. Number One, ilipikwa na Shady Clever. Nashangaa katika watu waliokwenda Kigoma kusherehekea miaka 10 ya Diamond kimuziki, Shady hakukwea gogo la kati (treni), wakati Number One ilimfungulia milango mingi Diamond.

Hiyo sio topic mama. Ikae pembeni tuyazungumze yenye kichwa na miguu; Number One ikazaa Number One Remix, humo ndani Diamond ‘alimuwekamo’ Davido, basi mzigo ulisambaa Afrika. Sijui kwa nini Davido hakwenda Kigoma kwenye miaka 10 ya Diamond? Inawezekana ilikosekana treni la kutokea Nigeria, maana gogo watu walipandia Kamata, Dar mpaka Mwisho wa Reli. Wanapaita Lwama (Kigoma).

Tuendelee na mjadala wetu wa siku; Number One Remix ikampeleka Diamond Platnumz ‘kuperform’ kwenye tuzo za Glo Caf 2014, zilizofanyika Eko Hotel and Suites, Victoria Island, Lagos, Nigeria, Januari 2015.

Halafu wakati huo Diamond alionekana ‘junia’ mbele ya wababe wa Afrika, Mr Flavour, P Square, Fally Ipupa na wengine ambao walipanda jukwaani kukinukisha. Hesabu, hiyo ni miaka mitano iliyopita.

Januari 5, 2017, ndio siku zilitolewa tuzo za Glo Caf 2016. Venue ni Ukumbi wa Kimataifa, Abuja, Nigeria. Kumbukumbu ya siku hiyo sio Riyad Mahrez alivyowakalisha Sadio Mane na Pierre Aubameyang, kushinda Mchezaji Bora Afrika. Kwa Bongo, big memory ni Diamond Platnumz.

Ndio, tofauti na Januari 2015, alipopanda jukwaani Eko Hotel and Suites, Lagos, akionekana ni underdog mbele ya Flovour, P Square, Fally Ipupa na wengine wote, Januari 2017, Diamond alikuwa mmoja wa big men katika show.

Diamond alichangia jukwaa na Flavour, Yemi Alade na wengine ambao kwake walikuwa ndio underdog. Hivyo, kama mwaka 2017, Diamond alipanda jukwaani kwenye tuzo za Glo Caf na kufanya kweli kama mmoja wasanii majina makubwa wenye kuuza shoo, yaani headliners, sasa inashitua nini katika tuzo hizohizo Januari 2020? Yaani miaka mitatu baadaye.

Iko hivi, Diamond kupiga shoo Glo Caf awards wala haistui. Kwake ni mambo ya kawaida sana. Inatakiwa wasanii wengine waone wivu kumwona mwenzao anazidi kuimarisha msuli wake kimataifa. Wafuate nyayo. Sio kung’aa macho tu.

SHOW SASA

Haimaanishi kwa sababu haishitui ndio Diamond asipongezwe, hapana! Anastahili “mipongezi ka’ yote”. Maana kufikia kilele inawezekana, lakini kubaki kileleni huhitaji msuli, nidhamu, kujitambua na kulitambua game.

Si hata dume la nyuki lililotumia msuli mkubwa kumpata malkia na kumpa ujauzito, baada ya hapo lilikufa? Halikungonja japo limhudumie malkia mjamzito, halikuwaona hata watoto wake. Halikushuhudia wala kufaidi matunda ya jasho lake.

Kitendo cha Diamond kupiga shoo Glo Caf 2014, kisha 2016 na kurudi tena za 2019, ni kipimo kwamba msuli wa Diamond sio kama wa dume la nyuki. Kwamba baada ya kufika kileleni ingekuwa basi. Janki bado anakaza. Kwani uongo? Hata supastaa wa kikapu Hasheem Thabeet, aliingia NBA kwa kishindo, lakini hakumudu kubaki kileleni. Akashuka na kupotea. Kiu ya Watanzania kumwona staa wao akipigana vikumbo na akina LeBron James, Steph Curry, Kevin Durant na wengine, haikuwahi kutibiwa.

Kwa nini tufichane? Hivi unajua yule 20% ni sampuli ya dume la nyuki? Alikusanya ‘miguvu’ weee! Mwaka 2011, Diamond Jubilee Hall kwenye Tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music 2010, si ndio 20% akafika kileleni? Akachukua tuzo tano kwa mkupuo. Na huo ndio ukawa mwisho wa kutamba.

20% hakufaidi matunda ya jasho lake lililomfikisha kileleni. Usela ukawa mwingi. Akaporomoka na kutoweka. Ni kama dume la nyuki maskini. Baada ya kumpa mimba malkia, watoto wakabaki kusimuliwa: “Baba yenu alikuwa shujaa. Alimpa mimba malkia.” Nasi tunasimuliana: “Asilimia 20 alikuwa wa moto, alifunika tuzo tano za Kili.”

Mwaka 2012, Diamond Platnumz alichukua tuzo saba Kilimanjaro Tanzania Music, lakini mpaka muongo wa tatu wa Karne ya 21 unaanza bado yupo anaballl. Yes, Diamond is balling to the game like never before. Utamwambia nini?

Hivyo, apongezwe kwa kazi nzuri ya kuendelea kukaza. Janki ana nidhamu na anajua mahitaji ya soko la muziki kulingana na wakati unavyobadilika.

TULE BURUDANI SASA!

Januari 7, mwaka huu, ndani ya Albatros Citadel Hotel, mjini Sahl Hasheesh, jijini Hurghada, tuzo za Glo Caf 2019 zilichukua nafasi na supastaa wa Senegal na Liverpool, Sadio Mane, alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Afrika.

Diamond alikuwepo kutumbuiza. Legend Samuel Eto’o ndiye alimtangaza kumwita jukwaani. Mondi bin Laden akaingia na ‘Tetema’ ambao alishirikishwa na janki aliyemkuza mwenyewe, Rayvanny.

Kisha, Diamond akapiga sebene la maana kwa ‘Yope’ ambayo ameshirikishwa na Mkongomani Innoss’B. Akafanikiwa kuamsha ukumbi mzima. Watu wote wazito walipanda jukwaani. Diamond akawachezesha.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino; Rais wa Caf, Ahmad Ahmad; Eto’o; Mane na wengine wote walipanda jukwaani kuinjoi huduma ya sebene kutoka kwa Simba wa Tandale.

Ilikuwa siku poa kwa Diamond. Maana shoo ilidhihirisha kuwa japo Diamond kuperform Glo Caf imekuwa kawaida kama vile msanii wa WCB kuperform Wasafi Festival, lakini kuna digrii zimeongezeka. Diamond wa Glo Caf 2016 anazidiwa sana na wa Glo Caf 2019.

Sema nini? Diamond anazingua na mi-playback yake. Jukwaa kama lile kuimba playback ni kupunguza thamani ya muziki. Hata bila live band, alishindwa vipi kuingia studio kutengeneza instrumental maalum ya kuperform Glo Caf?

Jukwaani ndio ofisini kwake. Zipo shoo waandaaji hawataki live band, lakini ndio uimbe playback? Tena wimbo wa kushirikishwa? Halafu unagandamizia mahali alipoimba Rayvanny na Innoss’B. Hiyo akili gani Simba? Hapa nakuvua cheo.

Kama uliona ile ngoma ya Innoss’B ndio ilibamba, kwa nini hakutengeneza instrumental ili Innoss’B asisikike kabisa, kisha yeye atambae na eneo lake? Alichokifanya Diamond sio professionalism kabisa.

Mbona Diamond ana ngoma nyingi kali? Badala ya Tetema ya Rayvanny, kwa nini hakupiga African Beauty? Inama? Baba Lao? Marry You? Kidogo? Mbona zipo nyingi? Aache mambo ya playback. Kama sio live band, awe anatengeneza instrumental maalum za kuperform jukwaani. Sio kututikisia mdomo wakati haimbi. Na ajiamini kwenye nyimbo zake, sio kung’ang’ana na za kushirikishwa.