Breaking News

DuduBaya awagomea Basata, atangaza kuachana na muziki

Tuesday April 14 2020

 

By Nasra Abdallah,Mwananchi [email protected]

Msanii wa Bongofleva nchini Tanzania,Tumaini Godfrey maarufu  Dudu Baya amegomea wito wa Baraza la Sanaa Tanzania(Basata).
Hii ni mara ya pili kwa Dudu Baya kuvutana na baraza hilo,ambapo Januari 7,mwaka huu walipomuita kuhusiana na kuweka video katika mitandao ya kijamii zikiwa na maneno yasiyokuwa  na staha,  aligoma kwenda hadi kufikia hatua ya kufungiwa kutojihusisha na sanaa lakini baadaye Februari, 2020  Waziri  wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kumsamehe.
Baada ya msamaha huo DuduBaya  aliahidi  kujirekebisha.
Sambamba na kugomea wito huo pia DuduBaya ametangaza kujifuta rasmi kuwa msanii kwa kile alichoeleza kutoridhishwa na figisufigisu zinazoendelea kwenye tasnia ya sanaa.
Amesema mbali na hilo pia  Basata haichukulii  hatua malalamiko mbalimbali ambayo wamekuwa akiyawasilisha kuhusu sanaa.
Hatua hiyo ya DuduBaya imekuja  baada ya Aprili 14, 2020 Basata kumwandikia barua ya wito ambayo ilisainiwa na katibu wa baraza hilo, Godfrey Mngereza.
Barua hiyo  ilimtaka kufika leo Jumanne Aprili 14 katika ofisi zao zilizopo Ilala Sharif Shamba,  saa 3:00 asubuhi.
"Wito huu umetokana  na wewe kuonekana katika mitandao ya  kijamii ukitumia lugha  zisizo za staha ukiwa kama msanii unayetakiwa kuzingatia maadili mema katika jamii.
"Ikumbukwe kuwa usipofika taratibu nyingine zitafuata kwa mujibu wa sheria ya baraza na kanuni zake bila ya kukupa taarifa nyingine, "ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Mwananchi ilifika ofisi za Basata saa 3:00 na kuelezwa kuwa msanii huyo bado hajafika na Hadi inaondoka eneo hilo saa tano asubuhi alikuwa hajafika jambo lililosababisha kumtafuta kujua sababu.
Akizungumza kwa njia ya simu, DuduBaya amesema ni kweli hajaenda kama alivyotakiwa na kueleza sababu kuwa wamemfungia akaunti ya Instagram.
Kutokana na hilo alimpigia Mngereza kumueleza namna alivyochukizwa kufungiwa hivyo  hata ofisini kwao hatakwenda tena.
“Mimi kuanzia sasa siyo msanii, nimejitoa rasmi katika sanaa, waambieni na nimeshawaambia”amesema DuduBaya.
Mngereza amesema kuwa wanaendelea na hatua nyingine na kufungiwa kwa akaunti ya instagram ya msanii huyo haiwahusu.
“Kujifuta usanii hakutuzuii kumchukulia hatua zaidi, hilo la kujitoa katika sanaa amelisema yeye na sisi tunafanya kazi yetu kwa mujibu wa sheria,”amesema Mngereza.

Advertisement