Breaking News

Harmonize kuwaleta Burna Boy na Morgan Herittage Uwanaj wa Uhuru

Tuesday March 17 2020

 

By Exaud Mtei, Mwananchi

Dar es Salaam. Baada ya Kufanikiwa kuweka historia mwishoni mwa wiki iliyopita kwa uzinduzi wa albamu  yake ya AFROEAST, Msanii Harmonize ametangaza kufanya onyesho kubwa Jijini hapa  katika uwanja wa Uhuru
Harmonize maarufu Konde Boy amewaambia wanahabari jana kuwa baada ya kufanya uzinduzi wa album katika ukumbi wa Mlimani City uliohudhuriwa na wageni waalikwa 500, amepokea malalamiko mengi ya watu ambao hawakupata nafasi ya kushuhudia uzinduzi huo.
“Nimeamua kufanya upya uzinduzi wa albamu hii katika Uwanja wa Uhuru Dar es salaam ili Watanzania wengi zaidi wapate nafasi ya kushuhudia kile kilichofanyika Mlimani City.
“Uzinduzi huo  utafanyika Juni  27, 2020 ambapo tiketi  zitaanza kuuzwa mapema mwishoni mwa mwezi huu huku akisema bei ya tiketi itakuwa ndogo ili kila Mtanzania aweze kushiriki,”amesema bila kuweka wazi bei ya tiketi hizo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Konde Gang wasanii ambao wameshirikishwa katika albamu  hiyo wa Tanzania na nje wote watakuwepo siku ya uzinduzi huo  jambo ambalo linatajwa kufanya siku hiyo kuwa kubwa zaidi.
Harmonize katika albamu hiyo ameshirikisha wasanii kutoka nje ya nchi kama Burna Boy, Yemi Alade, Phino, Skales, Mr Eaz wote kutoka Nigeria pamoja na Morgan Herritage kutoka Jamaica.
Kutoka Tanzania wamo wakongwe wa Bongofleva kama Lady Jaydee na  Mr Blue ambao wote kwa mujibu wa Harmonize wote watakuwepo siku ya uzinduzi huo.
“Uzinduzi huo utafanyika kama inavyokuwa matamasha, ambapo itaanza saa sita mchana na kuendelea hadi majogoo ili kuwapa nafasi wasanii wengi zaidi kutoa burudani.
“Nimepanga  kualika wasanii wengi wa Tanzania ambao walinitangulia katika tasnia, lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata burudani na nafasi ya kufurahia kinachofanywa na kijana wao,”amesema Harmonize.

Advertisement