Jamaika yatwaa taji la Miss World 2019

Muktasari:

Toni-Ann Singh  jana usiku aliipeperusha vema bendera ya Jamaica baada ya kutwaa taji la mrembo wa dunia ikiwa ni baada ya miaka 26 kupita tangu nchi hiyo kutwaa taji hilo

Toni-Ann Singh jana usiku aliipeperusha vema bendera ya Jamaica baada ya kutwaa taji la mrembo wa dunia.

Shindano hilo lilifanyika usiku wa kuamkia leo katika ukumbi wa ExCeL London nchini Uingereza.

Shindano hilo ambalo hii ni mara yake ya 69 kufanyika kwake kwa Tanzania mrembo Sylivia Sebastian ndiye aliwakilisha huku akifanikiwa kuingia kwenye 20 bora ya warembo wenye vipaji.

Hata hivyo pamoja na mambo mengine yaliyofanyika katika kusaka washindi wa vipengele mbalimbali katika shindano hilo, mwisho wa siku Toni-Ann Singh ndiye aliyetwaa taji hilo.

Singh mwenye miaka 23 ambaye ni mhitimu Chuo Kikuu cha Florida katika fani ya  saikolojia na wanawake, alipokea taji kutoka kwa Venessa Ponce De Leon, Mrembo kutoka nchini Mexico aliyetwaa taji hilo mwaka 2018.

Ushindi wa Toni-Ann Singh   unaifanya nchi ya Jamaica kutwaa taji hilo baada ya miaka 26 kupita na kuwa mara yake ya nne kulichukua tangu shindano hilo lianzishwe.

Katika mashindano hayo mshindi wa pili alikuwa mrembo kutoka Ufaransa, Ophely Mezino, wa tatu ni Suman Rao kutokea nchini India