EXTRA SPESHO: Jux, Vanessa kwani kuna mtu anateseka?

Sunday November 24 2019

 

By AMOUR HASSAN

NI ngumu hivi sasa kwa Juma Jux na Vanessa Mdee kuzungumzia muziki wao.

Ngoma zao kali na juhudi kubwa wanazofanya katika kujiendeleza kisanii ndani na nje ya mipaka, siyo vitu vinavyopewa nafasi kama ilivyo ishu ya kuvunjika kwa penzi lao na jinsi vile kila mmoja anavyojisikia katika penzi lake jipya. Jux ana ngoma mpya inayokwenda kwa jina la ‘Sugua’ aliyomshirikisha Diamond Platnumz. Ngoma inafanya vizuri. Inashika namba moja katika ngoma zinazotrend YouTube. Imeshapata ‘views’ zaidi ya milioni moja, licha ya kwamba ina siku tatu tu tangu video yake iachiwe. Vanessa pia ana ngoma mpya ‘Never Ever’ aliyoshirikiana na mwanamuziki wa Jazz kutoka Gabon, Frederic Gassita, iliyotoka siku tisa zilizopita. Inashika namba 40 kwenye ngoma zinazotrendi YouTube na imeangaliwa mara 206,000.

Wote wawili wana ngoma nzuri ambazo zinahitaji promo zaidi ili kupata mafanikio zaidi.

Na ukiacha ngoma hizo mbili, wawili hao ni wasanii wakubwa nchini, lakini bado wanahitaji nguvu katika kupenya zaidi kwenye gemu barani Afrika na hata duniani kwa ujumla. Lakini mijadala mikubwa inayowazunguka sasa ni kuhusu kuachana kwao. Na kuhusu wapenzi wao wapya. Jux ana mwanamitindo wa Thailand, Nayika (25) na Vanessa kanasa kwa muigizaji wa tamthilia inayohiti Marekani na kwingineko duniani kwa sasa ya Power, Olurotimi Akinosho a.k.a Rotimi (30). Kwenye tamthilia ya Power inayoandaliwa na rapa 50 Cent, Rotimi anaigiza kama kijana wa dili za kuuza dawa za kulevya akitumia jina la Andre Comeman ‘Dre’.

Jux na Vanessa wanaonekana kuwa na furaha katika maisha yao mapya ya kimapenzi, lakini bado kuna maneno ama matendo wanayofanya yanayoashiria kurushana roho. Kwa kuna anayeteseka?

Wiki hii, Vanessa na Jux wamefanya intavyuu kubwa za zaidi ya saa moja-moja. Katika mahojiano yake na MillardAyo, Vanessa alionyesha amekolea kwa Rotimi na anaonekana ana furaha zaidi.

Advertisement

Hata Millard alipomtaja Vanessa kama “Mama Akinosho”, kimwana huyo mwenyewe akakazia kwa kusema “Mrs Akinosho”.

Vanessa alisema licha ya kwamba kiumri amemzidi kijana huyo Mmarekani mwenye asili ya Nigeria kwa “miezi mitatu, minne”, lakini anajivunia sana kuwa naye kwa sababu Rotimi anampa “ushauri ambao hajawahi kupewa na mtu YEYOTE” na vile “ana uzoefu wa maisha kwa sababu ameishi Marekani”. Kimwana huyo pia amesema anajutia uhusiano wake uliopita kwa sababu alikuwa akiishi maisha “feki, feki, feki” na ya kujificha, mambo ambayo hayampendeza.

Licha ya kutomtaja moja kwa moja Jux, lakini kiwepesi tu unaweza kutafsiri kuwa anamrushia makombora mpenziwe huyo wa zamani waliyedumu pamoja kwa zaidi ya miaka mitano.

Jux na Vanessa waliwahi kuachana kipindi cha nyuma kabla ya kutangaza kurudiana kwenye jukwaa la Fiesta 2017.

Jux naye juzi Ijumaa usiku alialikwa katika kipindi cha ‘Block 89’ cha Wasafi FM ambacho hurushwa ‘live’ na Wasafi TV. Asilimia kubwa ya maswali yaliyoelekezwa kwake na watangazaji wa kipindi hicho yalihusu kuvunjika kwa penzi lake na Vanessa na anavyojisikia akimuona kimwana huyo anavyojiachia na staa wa Marekani.

“Kama binadamu, hata ukikutana tu na demu mtaani ukachukua namba yake, kisha kesho akakwambia ‘sitaki unipigie tena’ lazima utajisikia vibaya,” alisema Jux kuhusu anavyomtazama Vanessa katika uhusiano wake mpya.

Na kuhusu kuumia roho? “Hapana, siumii,” alijibu Jux.

Jux alikwepa swali kama walipanga kuoana na Vanessa na akakanusha uvumi kwamba moja ya sababu za kuachana kwao ilikuwa ni kimwana huyo kushindwa kumzalia mtoto.

“Hapana siyo kweli. Kuzaa ni mipango tu,” alisema Jux, ambaye daima amekuwa akimsifu Vanessa kuwa ni mwanamke mrembo na aliyekuwa akimshauri kwa mengi.

Alipoulizwa kama alitarajia Vanessa kuibukia kwa staa mkubwa wa Marekani, Jux alisema alitarajia kimwana huyo apate mpenzi mpya kwa sababu ni mrembo na anastahili mtu wa hadhi ya juu.

Jux akasema yuko poa kabisa na bebi wake mpya kutoka Thai, japo umbali kati yao unawafanya wasionekane pamoja mara kwa mara.

Kiujumla, ni ngumu kwa Jux na Vanessa kuzungumzia muziki wao kwa sasa. Mijadala kila kona ni kuhusu maisha yao binafsi. Watu Insta watampongeza Vanessa kwa ‘kukaa’ kwa supastaa lakini wapo pia watakaomshambulia kwa kusema “ushauri anaopewa na Rotimi hajawahi kupewa na mtu YEYOTE” au kusema Rotimi ana uzoefu wa maisha KISA kaishi Marekani.

Promo za uhusiano wa kimapenzi zinasaidia sana kiki ya msanii. Lakini TAHADHARI. Uhusiano na watu wengine si jambo ambalo Jux na Vanessa wana uamuzi nalo kwa asilimia 100. Ni fifte-fifte. Kwa sababu ni lazima yule mtu mwingine akolee kama ulivyokolea wewe. Vinginevyo, akikata kamba na umeshaingia kichwa na miguu, inaweza kukuacha na msongo mkubwa wa mawazo na kuleta athari katika kazi yako. Tunawapenda Jux na Vanessa kwa kazi zao. Tunapenda kuona wakizidi kupaa kisanii. Ndio maana leo tunawashauri waingie huko walikoingia kwa tahadhari.

Advertisement