Kenny: Hatukuiga video ya wimbo Gere, ni makubaliano

Saturday February 22 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya kusambaa kwa picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha namna vipande vya video ya  wimbo wa Gere  vilivyofanana na wimbo Brisa wa msanii Iza,  Kenny ambaye ni mwongozaji wa video hiyo amekanusha madai hayo.

Wimbo Gere umeimbwa na Tanasha Donna aliyemshirikisha mpenzi wake, Diamond Platnumz.

Kenny  aliyeshinda  tuzo ya Afrima ya mwongozaji bora wa video mwaka 2019 amesema, “hakuna kilichofanyika tofauti, hayo yalikuwa ni makubaliano kati yetu na Iza. Diamond hawezi kutumia wazo la mtu bila kumpa taarifa na si jambo la ajabu katika sanaa, linafanyika sana.”

Donna aliuweka wimbo huo mtandaoni Februari 19, 2020 na tangu siku hiyo Iza ambaye ni raia wa Brazil amekuwa akimshutumu Diamond kuiga video hiyo kinyume na makubaliano yao.

Iza  ambaye jina lake halisi ni Isabela Cristina Correia de Lima alieleza kuwa aliombwa wahusika kutumia wazo la video yake, lakini kilichofanyika ni kama kahamisha wazo zima.

Ukitazama video ya Brisa, Iza anaonekana kuwa katika maeneo tofauti yanayofanana na yaliyopo katika video ya Gere.

Advertisement

Babu Tale ambaye ni meneja wa Diamond alipoulizwa kuhusu suala hilo amesema anaonewa kwa kuwa si mtayarishaji wa video hiyo.

“Muulizeni  mwongozaji aliyesimamia utayarishaji wa video hiyo,” amesema.

 

Advertisement