Sauti za Busara na kampeni kupinga Unyanyasaji wa Kijinsia

WAKATI wasanii wa Afrika wakitarajiwa kutoa burudani kwenye tamasha la  Sauti za Busara 2020 kaulimbiu ya mwaka huu kwenye tamasha hilo ni ‘Pandisha Sauti Yako, Sema Hapana kwa Unyanyasaji was Kijinsia’.
Tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuanza Februari 13 hadi 16 mwaka huu Mji Mkongwe kisiwani  Unguja ambapo Mkurugenzi wa tamasha hilo  Yusuf Mahmoud, amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kubadili mitizamo, kuanzisha mazungumzo na kuhamasisha heshima kwa wanawake kwa kuongeza uhamasishaji juu ya unyanyasaji wa kijinsia.
Yusuf amesema hii ni muhimu ili kuleta mabadiliko ya tabia na kwasababu hiyo, ujumbe unaolenga suala hilo utafikia tamasha zima kwa ujumla.
“Wasanii wengi wa tamasha, ndani na nje ya nchi wamekubaliana kuhakikisha kuwa kampeni hii
inafanikiwa kuunganisha watazamaji wa tamasha hapa Tanzania na kwingineko, alisema Mahmoud.
Amesema tamasha limeandaa shughuli zinazolingana za kukuza mifano ya jinsia, kama vile mafunzo ya usimamizi wa jukwaa kwa wanawake, itakaoongozwa na mtaalamu kutoka Zimbabwe, Ushirikiano wa kisanii wa Swahili Envcounters, Circus4Life na vikundi vingine vya wanawake
“Jukumu letu kuu kama waandaaji wa tamasha ni kusaidia kujenga ustadi na uwezo kwa Watanzania katika tasnia ya muziki. Ninazungumzia wasaani wakiwa jukwaani na pia watu wengine  nyuma ya pazia: wasimamizi, wazalishaji, sauti na mafundi wa taa na kadhalika.”
“ Hivi sasa nchini Tanzania, wanawake wachache ndio wanaojitokeza kuingia kwenye muziki wa asili na hii ndio sababu tamasha la Sauti za Busara 2020 tumealika wasanii kama Siti the Band (Zanzibar), Diarra na Mamy Kanouté (kutoka Afrika Magharibi), Pigment (Reunion), Evon na Apio Moro (Uganda), Circus4Life kutoka Bagamoyo na DJs kutoka Afrika Mashariki
Mahmoud amesema tamasha lina imani wasanii hawa wanaoshiriki watatoa msukumo, kutoa matumaini na motisha kwa wanawake na wasichana wengi ambao wanaweza pia kuzingatia kazi ya muziki
Tamasha  hili la Sauti za Busara ni la  17 kufanyika mwaka huu na linadhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Africalia, ubalozi wa Uholanzi, Bristish Council, Zanzibar Media Corporation, Zanlink, Memories of Zanzibar Ubalozi wa Ufaransa, Emerson Zanzibar, Radio ya Chuchu FM, Mozeti, Music in Afrika.