VIDEO: Tamasha la Jamafest linavyokonga watazamaji

Monday September 23 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam. Ngoma za asili za mataifa ya Afrika Mashariki zimeonekana kuwa kivutio katika tamasha la utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest) linaloendelea katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Idadi kubwa ya wakazi wa jiji hilo wamejitokeza kutazama burudani iliyokuwa ikitolewa na wasanii wa nchi zinazounda jumuiya hiyo ambazo ni Tanzani, Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.

Kila kikundi kinachopanda jukwaani kinaonyesha umahiri mkubwa jambo linalowafanya watazamaji kuendelea kutazama.

Licha ya kuwa eneo la watazamaji halikuwa na viti wala turubai watu walisimama kuanzia asubuhi hadi muda huu bila kujali jua kali linalowaka uwanjani hapo.

Akizungumza na Mwananchi mkazi wa Kurasini, Clementine Chale amesema ameshawishika kufika hapo baada ya kuona kwenye runinga burudani inayotolewa.

“Binafsi nilikuwa sifahamu nimeona jana kwenye tv, nikaona nije nijionee kwa macho kwa kweli Afrika tumebarikiwa. Leo nimeona ngoma za kila aina kwa kweli nimefurahi,”

Advertisement

“Nimeguswa zaidi na wenzetu wa Burundi wanavyopiga ngoma zao, yaani inatamanisha kuendelea kuangalia, Wakenya nao wako vizuri hata Tanzania nimeona kumbe tuna wasanii mahiri wa utamaduni,” amesema

Mary Wambua ambaye ni mjasiriamali kutoka Kenya amesema tamasha hilo limekuwa chachu ya mataifa hayo  kujifunza tamaduni za wengine.

“Si mara ya kwanza nakuja Tanzania ila safari hii imekuwa nzuri zaidi pamoja na kukutana na wajasiriamali wa Afrika Mashariki, nimeona ngoma za asili za kuvutia.”

“Watoto wanacheza kwa kujiamini hii inaleta raha na inapendeza kuona tunarithisha vizazi vyetu tamaduni zetu,” amesema Wambua

Advertisement