Wasanii wa Reggae Jhikoman na Dabo wakwama Uganda kwa kukosa nauli

Monday November 25 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Wasanii wa muziki wa Reggae nchini Tanzania, Jhikoman na Dabo wamekwama nchini Uganda walikokuwa wamekwenda kushiriki tamasha la Reggae lijulikanalo kama  ‘Reggae on Nil’.

Tamasha hilo lilifanyika Novemba 21 hadi 23, 2019 na baada ya kumalizika na wasanii kutakiwa kuondoka, mwandaaji anayetambulika kwa jina la Madgunz anadaiwa kuwa kaingia mitini huku simu zake zikiwa hazipatikani.

Mmoja wa wasanii aliyejitambulisha kwa jina la Gotta Irie, ameiambia Mwananchi leo Novemba 25, 2019 kuhusu mkasa huo na yeye namna alivyofanikiwa kuondoka.

Katika maelezo yake, Irie amesema alienda siku moja kabla ya tamasha na katika mkataba walioingia na mwandaaji, alimlipa kila kitu.

“Lakini na mimi nilijiongeza kwa suala la usafiri wa kwenda na kurudi, nilikuwa nimeshakata tiketi mapema,” amesema mwanamuziki huyo.

 

Advertisement

Hata hivyo, amesema kwa upande wa kina Jhikoman ambao waliongozana na wake zao, walikwenda siku mbili kabla ya tamasha na walikatiwa tiketi na mwandaaji za kwenda tu.

“Suala la wenzangu kukwama kurudi nimelisikia baada ya mimi kuwa tayari nimesharejea nchini leo, na kikubwa hapa ni malipo yao hawajamaliziwa na kupewa tiketi za kurejea walikotoka.

“Hata hivyo, bado nafuatilia suala hilo na muda mfupi niliwasiliana na Jhikoman ambaye aliniambia bado wanamtafuta mwandaaji na amesema kuna wanamuziki wengine wakiwemo wa Kenya wanashikiliwa na Jeshi la Polisi,” amesema Irie.

 

Kupitia kundi la Whatsup la wasanii walioshiriki tamasha hilo, mmoja wa wasanii amesema zaidi ya wasanii 25 wamekwama nchini humo.

Mwananchi imeutafuta uongozi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata)  ili kujua kama wana taarifa za kukwama kwa wasanii hao, lakini simu ya Katibu Mtendaji, Godfrey Mngereza imekuwa ikiita tu bila  kupokelewa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.

Advertisement