MTAZAMO WANGU : Sakata la uhaba wa Sukari, hongera JPM lakini…

Muktasari:

  • Katika mtazamo huo nilieleza wazi tatizo la uhaba wa sukari ambalo lilianza kujionyesha tangu Machi, mwaka huu kama lisipopewa uzito unaostahili linaweza kusababisha madhara kwa Watanzania.

Machi 13 mwaka huu, niliandika katika safu hii kuwa watendaji wa Serikali wanasubiri Rais John Magufuli afanye ziara ya kushtukiza kwa wauza sukari ndiyo wachukue hatua na kuwadhibiti wanaoficha bidhaa hiyo muhimu.

Katika mtazamo huo nilieleza wazi tatizo la uhaba wa sukari ambalo lilianza kujionyesha tangu Machi, mwaka huu kama lisipopewa uzito unaostahili linaweza kusababisha madhara kwa Watanzania.

Nilieleza wazi viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, wakuu na mikoa na maofisa biashara wanawajua wauza sukari na wanajua maghala yao ya kuhifadhi bidhaa hiyo, lakini hawawezi kuwabana wafanyabiashara hawa.

Nilifafanua vigogo hawa wanakosa ujasiri wa kufanya uamuzi kwa kuwa wanajua wafanyabiashara ndiyo wafadhili wao, wanajua wafanyabiashara ni makada wa chama chao, hivyo hawagusiki.

Leo miezi miwili tatizo la sukari limekuwa kubwa kila kona ya nchi wananchi wanalia hakuna sukari na bei imepanda kutoka kilo Sh1,800 hadi zaidi ya Sh3, 000.

Hata hivyo, baada ya agizo la pili la Rais Magufuli alilotoa Mei 6 akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Arusha la kuwasaka wote walioficha sukari ambao ni sawa na wahujumu uchumi, tunaona viongozi wa Serikali wakianza kuhaha na kuwafuata wafanyabiashara na kuwasihi waitoe bidhaa hiyo.

Kinachoendelea sasa baadhi ya viongozi wamejaa hofu ya kutumbuliwa na Rais Magufuli, hivyo wanawafuata wafanyabiashara wakiwa mikono nyuma na kuwasihi kufichua sukari waliyoficha na kuwabembeleza wauze kwa bei elekezi ya Serikali.

Kuna viongozi wengine wamekaa kando na sasa wanatumia maofisa wao wa chini kuvamia maghala ya wafanyabiashara hawa na kuwalazimisha kuitoa sukari ambayo wameificha.

Hadi sasa zaidi ya tani 10,000 zimekamatwa jijini Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Mtwara na Arusha na bado kunaelezwa kuwa sukari nyingine imehifadhiwa maeneo mbalimbali nchini.

Tukio hili limewafumbua macho Watanzania wengi na kuona udhaifu wa baadhi ya watendaji wa Serikali wanaoshirikiana na wafanyabiashara na pia jeuri ya baadhi ya wafanyabiashara.

Kwa mazingira haya, wengi tunaunga mkono jitihada za Rais Magufuli kutangaza vita na kikundi cha wafanyabiashara wakubwa wasiozidi 10 ambao wamehodhi biashara ya sukari, lakini wengi tunataka vita hii iwaguse na maswahiba wao.

Rais Magufuli anasema atapambana na wafanyabiashara hao hadi mwisho wake na kwa kuonyesha kuwa ana dhamira ya kweli kufanya hivyo, tayari Serikali imeanza kuingiza nchini sukari tani 70,000 ili kukabiliana na upungufu uliopo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kati ya tani hizo 70,000, tayari 11,957 zimewasili nchini na zimeanza kusambazwa na tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya kaskazini.

Waziri Mkuu akaongeza kuwa, tani 3,000 zitapelekwa Kanda ya Ziwa, 2,000 mikoa ya Kusini, 2,000 Nyanda za Juu Kusini na tani 2,000 Kanda ya Kati.

Katika mpango huo, tani nyingine 24,000 za sukari zilitarajiwa kuwasili Ijumaa wiki hii na nyingine 20,000 zitawasili baadaye au mwishoni mwa mwezi au mapema mwanzoni mwa Juni.

Nirejee kusema, sakata la sukari limetuonyesha upungufu mkubwa serikalini; kwanza, kukosekana takwimu sahihi za mahitaji ya sukari na upungufu uliopo na pili, uwapo watendaji dhaifu wa Serikali ambao wanawaogopa wafanyabiashara, lakini tatu, kuna kundi kubwa ambalo linanufaika na biashara haramu ya sukari.

Vilevile, sakata hili la sukari limeibua maswali mengi kutokana na kauli za Rais Magufuli kuwa Watanzania wamekuwa wakilishwa sukari iliyomaliza muda wake inayotolewa katika mataifa kadhaa, ikiwamo Brazil.

Sukari inayokaribia kumaliza muda na wafanyabiashara wetu hudaiwa kuibeba na kuleta nchini na hivyo kuathiri afya za Watanzania wengi.

Binafsi naamini kauli hiyo ya Rais imekuja baada ya kufanya uchunguzi. Jambo la kujiuliza kwa miaka yote walikuwa wapi watendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)? Watendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)? watendaji wengine wa Wizara ya Afya na ile ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Mapato hadi kuruhusu Watanzania kulishwa sukari mbovu?

Mungu ibariki Tanzania.

0754296503