UCHAMBUZI: Tumekubali vijana wawe sawa na kuku wa kienyeji?

Niliwahi kuandika siku za nyuma kuhusu mitazamo potofu waliyonayo vijana wengi wa Kitanzania kuhusu maisha.

Nilieleza kuwa wengi wanatamani kupata mafanikio ya kimaisha kwa kutumia njia za mkato.

Nikatoa mfano wa kushamiri kwa harakati za vijana kucheza michezo ya kamari hasa ule wa kubashiri matokeo ya mpira wa miguu, maarufu kwa Kiingereza kwa jina la betting.

Nimesikia ulevi huo umewakumba hata watu wazima na wasomi, kila mtu sasa anataka ‘kubeti’.

Kwa kiasi kikubwa lawama nilizipeleka kwa vijana wenyewe nikiwananga kuwa hawajihimu kubadili mitazamo kuhusu maisha, mitazamo ya kujali kazi badala ya ile ya kutafuta maisha kwa njia za mkato ambazo nyingi zinawagharimu maisha yao.

Hofu yangu ni kuwa wakati vijana wa Kitanzania wakiendelea kujisahau, wenzao wa nchi jirani wanachangamka; leo vijana wa Kenya na Uganda na nchi nyingine za jirani, wanaingia nchini na kuzichukua fursa ambazo vijana wa Kitanzania wamezipa kisogo.

Huo ulikuwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine lazima tukiri kuwa hapa walipo vijana wenzangu wamefikishwa, hawakujifikisha wenyewe.

Kuna watu wanachekelea kuona hali hiyo huku wakitamani vijana wazidi kuangamia ili wazidi kuwatumia katika harakati zao zikiwamo za kisiasa.

Kwangu vijana wamefika walipo kwa sababu ya mfumo wa nchi yetu, mfumo umewasahau vijana. Pengine nirahisishe kwa kusema Serikali imewasahau vijana, hawana mtu au chombo cha kuwapa dira, wamekuwa kama kuku wa kienyeji wanaozuruza ovyo.

Kama kuku wanavyozurura kutwa nzima na mwishowe kurudi bandani wakiwa na maradhi, ndivyo walivyo vijana wa Kitanzania. Wamegubikwa na maradhi kuanzia matumizi ya dawa za kulevya, wizi, uhuni na kila aina ya ufedhuli.

Inawezakana vijana hawataki kazi lakini je, wamewezeshwa wakakataa? Uwezeshaji hapa si lazima wa kuwapa mitaji, bali hata ule wa kupandikiza fikra mpya vichwani.

Naomba kukumbusha ila sijui kama kuna matamasha na makongamano kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na hata taifa, yanayolenga kuwajenga vijana kama umma uliosahaulika nchini.

Ninayoona mimi ni matamasha ya burudani ambayo mengi hayana tija. Kwanza ndiyo chanzo cha uhayawani kwa vijana.

Sisemi hayapo kabisa, lakini hayo yaliyopo yana athari gani kwao, na kwa nini yasichukue ukubwa na msisitizo kama ilivyo kwa matamasha ya kipuuzi?

Natambua kuwapo kwa baadhi ya kampuni na asasi za kiraia zinazozunguka maeneo mbalimbali na kuwakusanya vijana wachache kwa mazungumzo

Hata hivyo, sikumbuki kuona programu ya maana yenye sura ya kitaifa inayoratibiwa na Serikali inayolenga kuwakomboa vijana.

Kama watu na kampuni binafsi wanaweza kuanzisha programu za kuwainua vijana, Serikali yenye kila aina ya rasilimali inashindwaje kubuni programu za kitaifa kwa manufaa ya umma mpana wa vijana?

Miaka ya hivi karibuni kulizuka mtindo wa vijana kuwa na makambi. Ulishamiri sana katika jiji la la Dar es Salaam. Vijana walipanga mawe na matairi mitaani, wakaanzisha bustani katika maeneo wanamoishi, wakabandika vitambaa na kujitambulisha kwa majina ya kambi zao.

Hii ilikuwa fursa nzuri kwa wizara inayoshughulika na ajira na wadau wengine kuwadaka vijana hawa na kuwapa maarifa. Haikuwa hivyo, tukawaacha wakawa wanatumia vijiwe hivyo kama maeneo ya kukusanyikia na kwenda ‘pikniki’ ufukweni.

Tungekuwa makini kama jamii, kambi hizi zingeanzishwa kwa wingi mjini na vijijini, tukazitumia kuwafunza vijana na kuwawezesha kuanzisha miradi midogomidogo, kuwapa elimu ya masoko na masuala mengine muhimu kwa ustawi wa maisha yao.

Hata hivyo, jukumu la kuwaokoa vijana ni letu sote kuanzia wazazi, walimu shuleni, Serikali, asasi za kiraia na jamii kwa jumla, sote tuna wajibu wa kubadili fikra za vijana.

Inawezekana tumekosea katika mfumo wetu wa elimu, watunga sera za elimu na mitalaa watusaidie ili wanafunzi wa Kitanzania waanze kunolewa kwa mtazamo mpya wa kupenda kazi tangu wakiwa wadogo.

Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kupigia chapuo mafunzo ya ufundi, stadi za maisha, ujasiriamali na uoanishaji wa masomo ya darasani na uhalisia wa maisha.