Waraka wa Pasaka wazua mazito KKKT

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo akiongoza maandamano kabla ya kuanza kwa ibada. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Waraka huo pia ulisababisha maaskofu wa dayosisi tatu kutengwa na Baraza la Maaskofu baada ya kutotekeleza maelekezo ya kuusoma kwa waumini wake wakati wa ibada.

Dar es Salaam. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limepewa siku kumi kufuta waraka wake wa Pasaka uliotolewa Machi 24, ambao mbali na masuala ya kiroho, ulitaja changamoto tatu za kijamii.

Waraka huo pia ulisababisha maaskofu wa dayosisi tatu kutengwa na Baraza la Maaskofu baada ya kutotekeleza maelekezo ya kuusoma kwa waumini wake wakati wa ibada.

Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la “Taifa Letu Amani Yetu” na kusainiwa na maaskofu 27, ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka kama Katiba mpya.

Lakini barua iliyosambaa jana mitandaoni na inayoonyesha imeandikwa Mei 30 na Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa mwenyekiti au askofu mkuu wa KKKT, inatoa maelekezo ya kufutwa kwa waraka huo kwa maelezo kuwa chombo kilichotoa tamko hilo hakitambuliki kisheria na Ofisi ya Msajili.

Hata hivyo, si Hamad Masauni (naibu waziri wa Mambo ya Ndani), Project Rwegasira (katibu mkuu wa wizara hiyo), wala Dk Hassan Abbas (msemaji wa Serikali) aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo, lakini katibu mkuu wa KKKT alithibitisha kupokea barua hiyo.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya,” inaeleza barua hiyo.

“Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia nyingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’. Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea barua hii, vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii.”

Barua hiyo inaonyesha imesainiwa na mtu anayeitwa M.L. Komba kwa niaba ya msajili.

Alipoulizwa na Mwananchi jana kuhusu suala hilo, katibu mkuu wa KKKT, Brighton Killewa alithibitisha kupokea barua ya msajili na kueleza kuwa baadhi ya maagizo yalishafanyiwa kazi.

“Ni kweli tulipokea wito wa msajili na mkuu wetu wa kanisa hakuweza kwenda kwa kuwa alikuwa na udhuru, lakini aliteua askofu wa kumwakilisha. Mimi na mwanasheria wa kanisa tulifika mbele ya msajili Mei 29,” alisema Killewa.

“Msajili alitupokea na akatupa mambo ya kuyafanyia kazi na ofisi ya katibu mkuu imeshayafanyia kazi baadhi na inaendelea kuyafanyia kazi mengine.

“Kwa sasa itoshe tu kusema kuwa tumeipokea barua na maagizo ya Serikali. Sasa nini tutafanya baada ya kupokea barua hiyo ni baada ya kukaa na kutafakari katika vikao vya kikatiba vya kanisa.”

Kwa mujibu wa tovuti ya KKKT, Lutherani inaongozwa na mkuu wa kanisa ambaye huchaguliwa kutoka miongoni mwa maaskofu kila baada ya miaka minne.

Vyombo vya maamuzi vya KKKT ni Mkutano Mkuu, ambao huundwa na maaskofu wa dayosisi zote 27, makatibu wa dayosisi na wakurugenzi wa taasisi za kanisa na chini yake kuna sekretarieti ambayo huongozwa na katibu mkuu.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Dk Abbas alisema: “(Hayo ni) Mambo ya kisekta ambayo hayahusiani na sera, yako chini ya sekta husika. Kwa kuwa sekta hizo zina wasemaji wake, mara nyingine si lazima mimi kuyafahamu. Hivyo, watafute wahusika kwenye sekta hiyo wathibitishe.”

Naye Masauni alikuwa na jibu tofauti. “Barua zote za wizara zinazohusu utekelezaji wa sera huandikwa na katibu mkuu. Hivyo, mtafute katibu mkuu au mtu aliyesaini barua hiyo kwa niaba yake athibitishe na kufafanua mambo mbalimbali,” alisema.

Na Rwegasira alisema yuko likizo tangu Juni Mosi, hivyo kuelekeza atafutwe naibu wake Yahya Simba.

Hata hivyo, Simba na msajili wa Vyama vya Kiraia, Mary Komba hawakupatikana.

Barua iliyosambaa jana inarejea nyingine za Mei 10 na Mei 22 na kikao kilichofanyika Mei 29 kati ya KKKT na Ofisi ya Msajili Wizara ya Mambo ya Ndani ikisema Askofu Mkuu KKKT ameshindwa kutii wito wa kufika Ofisi ya Msajili, kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 33 cha Sheria ya Jumuiya Sura 337.

“Kufanya hivyo ni kosa la jinai na bado unahitajika kufika mbele ya Msajili wa Vyama,” inasema barua hiyo.

Barua hiyo inasema taasisi inayoongozwa na askofu huyo imethibitika kutotekeleza masharti ya usajili kwa kushindwa kulipa ada za mwaka, kutoa taarifa za mikutano, za fedha na mabadiliko mbalimbali, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria hivyo anaelekezwa kutekeleza masharti ya usajili yote kama yalivyo.

“Fika Ofisi ya Msajili upewe madeni ya ada na malimbikizo yake ambayo unapaswa kulipa ndani ya siku saba (7) baada ya kupokea barua hii. Ijulishe Ofisi ya Msajili mabadiliko ya uongozi mliyofanya, kama yapo tangu mara ya mwisho kuwasilisha mabadiliko hayo Ofisi ya Msajili kwa barua na kwa kujaza fomu namba SA 6 ndani ya siku saba (7)” inasema barua hiyo.

Barua hiyo inaeleza hadi ilipoandikwa, katiba inayotambulika kutumiwa kuongoza taasisi ni iliyoandaliwa mwaka 1960 na kupitishwa na kukubaliwa na Ofisi ya Msajili mwaka 1963.

“Mnapaswa kuomba ridhaa ya Ofisi ya Msajili ya kurekebisha katiba kwa kujaza fomu husika mkikubaliwa muweze kupewa maelekezo ya kufuata ili kurekebisha katiba yenu ya mwaka 1963,” inasema barua hiyo.

Inasema Ofisi ya Msajili imejiridhisha kuwa taasisi hiyo imeunda chombo kisicho cha kisheria kinachoitwa “Baraza la Maaskofu la Kanisa la KKKT” na imetoa waraka ulioweka majina ya maaskofu na kusambazwa kwa umma wa Tanzania, kinyume cha sheria.

Inasema waraka haukuwa na lengo zuri kwa vile umehusisha masuala ambayo yapo nje ya imani, wakati KKKT ilikuwa na nafasi ya kuishauri mamlaka ya nchi au kuzishauri mamlaka za Serikali kuhusu ilichokiona ndani ya jamii, badala ya kutoa maandishi kwa umma.

Inasema Ofisi ya Msajili inaona ujumbe huo unaweza kuamsha hisia kwa jamii na kuleta tafsiri mbalimbali zenye mitazamo tofauti na mwelekeo mbaya kwa jamii na Taifa kwa jumla,” inasema barua hiyo.

Inasema kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Vyama Sura 337, na kwa vile baraza hilo halitambuliki kisheria katika Ofisi ya Msajili, Askofu Mkuu KKKT anaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi hiyo haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile ilichofanya.

“Tafadhali zingatia maelekezo uliyopewa kwa wakati. Ofisi inasisitiza kufuata masharti ya usajili mliyopewa wakati mnasajili taasisi yenu na kutunza amani na utulivu wa Watanzania,” inasema barua hiyo.