RIPOTI MAALUMU: KUPOTEA KWA BEN SAANANE

Ben Saanane

Dar es Salaam. Ni kimya kimetawala Kitongoji cha Hiti kilichojificha katikati ya mashamba ya migomba, kahawa na miti mikubwa.

Ni katika miteremko ya Mlima Kilimanjaro wilayani Rombo ndiko kinakopatikana Kijiji cha Mrere.

Sauti pekee unayosikika ni ya upepo unaovuma katika migomba, sauti za wanyama na watoto wanaocheza maeneo ya karibu.

Renatha Saanane, 54, mama mzazi wa Ben Saanane, anaendelea na shughuli zake za kila siku za nyumbani, lakini inambidi asimame na kumkaribisha mgeni ambaye ujio wake ametaarifiwa dakika chache zilizopita.

Uso wake hauna tabasamu ya kawaida anayopaswa kuwa nayo kwa wageni. Uchungu alioubeba moyoni mwake kwa zaidi ya miezi tisa baada ya kutoweka kwa mtoto wake wa kwanza, Ben Saanane, unasomeka waziwazi usoni kwake.

“Sijui kama ameuawa, ametekwa au anashikiliwa na vyombo vya ulizi na usalama. Hili naiachia serikali,” anasema Bi Saanane. Baadaye machozi yanachuruzika kwa muda lakini anajikaza na anajipa nguvu na kuendelea kujadili fumbo la kupotea mwanaye.

Mara ya mwisho kuongea na mwanaye ilikuwa ni Novemba 11 mwaka jana, siku tatu tu kabla Ben hajatoweka. Waliongea masuala mbalimbali, ikiwamo maandalizi ya harusi ya ndugu yao aishiye Dodoma.

“Hayo ndiyo mawasiliano yangu ya mwisho na yeye,” anasema, na kuongeza kuwa kwa kawaida hakuwahi kuingiwa hofu kuhusu ukimya wa muda mrefu wa mwanaye, ikizingatiwa kuwa nafasi yake kama msaidizi wa karibu wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ilimfanya awe na shughuli nyingi.

Kwa siku kadhaa zilizofuata baada ya kuongea na mwanaye kwa simu kwa mara ya mwisho, Bi Saanane aliendelea kumpigia Ben mara kwa mara lakini hakufanikiwa kumpata. Alichukulia hali hiyo kama jambo la kawaida.

Hata hivyo, anasema, kwa mshangao alijua baadaye kuwa hata mdogo wa Ben aitwaye Erasto na dada yake Agripina ambao pia wanaishi Dar es Salaam, pia hawakuweza kumpata kwa njia ya simu licha ya kumpigia mara kwa mara.

“Hapo wote tukaanza kuwa na wasiwasi lakini wengine wakaamini anaweza kuwa amesafiri nje ya nchi au maeneo yasiyofikiwa na mtandao wa simu ukizingatia uanaharakati wake wa kisiasa,” alisema Renatha.

“Bado hatukuweza kupata jibu, lakini wasiwasi wetu ulizidi baada ya suala la kutoonekana Ben liliripotiwia polisi Dar es Salaam na baadaye kuanza kuandikwa magazetini.”

Mama Saanane hafichi juhudi zilizofanywa na familia yake kumtafuta mwanaye baada ya taarifa za vyombo vya habari kujirudiarudia kwamba anaweza kuwa ametekwa.

Mara ya mwisho mwanasiasa huyo kijana wa upinzani kufika kijijini kwao, kwa mujibu wa mama yake, ilikuwa kati ya Agosti au Septemba mwaka jana alipokwenda kumzika bibi yake.

Suala la kupotea kwa Ben halikuchukuliwa kwa urahisi katika kijiji chake cha Mrere kilicho Kata ya Mashati, takriban kilomita 60 kutoka Moshi na Wilaya ya Rombo kwa jumla.

Wananchi wa kawaida katika eneo hilo wana ufahamu wa kutosha kuhusu hali ya kisiasa nchini na mara nyingi viongozi wa kisiasa wamejikuta wakikamatwa na kushtakiwa wakituhumiwa kutotii mamlaka, uchochezi na mambo kama hayo.

Ben mwenyewe hakuwa mgeni na siasa za Rombo. Wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 aligombea ubunge jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema na kushika nafasi ya pili baada ya kushindwa na mbunge wa sasa, Joseph Selasini (Chadema) katika kura za maoni.

“Anajulikana na watu wengi kwa sababu alikuwa machachari wakati wa kampeni,” anasema mama yake, akiongeza kuwa kutoweka kwake kuliwagusa watu wengi pia.

Baba yake, Focus Saanane, 63, anasema anaumizwa na kutoweka kwa mtoto wake lakini anainyooshea Serikali kidole cha lawama kwa jinsi walivyoshughulikia suala hilo.

“Tunaiachia Serikali kila kitu. Taarifa kutoka mamlaka hazijawahi kuwa za kuaminika,” anasema katika mahojiano mjini Moshi anakofanya biashara.

Anaonyesha kuwa familia yake inazidi kupoteza matumaini ukizingatia juhudi walizofanya bila ya mafanikio za kumtafuta kijana wao, ambaye licha shughuli zake ndani ya Chadema alikuwa pia akisomea shahada ya uzamivu ya uchumi.

Mzee Saanane anasema japokuwa Ben alilelewa na kukua kama mtu mwenye uhuru wa kwenda popote alipotaka, anazidi kukerwa na taarifa zinazokinzana kuhusu kutoweka kwake.

“Hatujui kama yuko hai au la. Mara ya mwisho kukutana naye ilikuwa wakati wa mazishi ya bibi yake,” anasema.

”Na ilikuwa mara ya mwisho kusikia kuhusu mwanangu. Familia inaumia sana lakini hatuna la kufanya. Mama yake ana uchungu mkubwa kijijini. Sisi kama familia kubwa tumejaribu sana kumsaka lakini hakuna mafanikio

Mzee Saanane anasema namba ya simu ya Ben ya Vodacoma imezuiwa na hawezi kujua mwanaye aliwasiliana na nani mara ya mwisho kabla ya kutoweka. Suala la kupotea kwake liliripotiwa kituo cha polisi Tabata jijini Dar es Salaam.

Anaisihi Serikali isaidie katika kumtafuta mtoto wake na kuwaondolea wasiwasi wa wapi alipo na usalama wake, akisema hata maofisa wa Chadema hawajatoa msaada wa kutosha katika kumtafuta mwanaye kama wanavyoonekana pia kuchanganyikiwa.

Godbless Lema, mbunge wa Arusha Mjini ni kiongozi pekee wa juu wa Chadema aliyewahi kumtembelea Mzee Saanane nyumbani kwake Moshi kumtuliza na kujaribu kutafuta namna ya kulifumbua fumbo hilo, anasema mzee huyo.

Inataendelea kesho