VIDEO: Baba wa mfanyabiashara Mo Dewji asimulia alivyompata mwanaye

Muktasari:

Gullam Dewji Hussein, baba wa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amesimulia jinsi alivyompata mwanaye aliyetekwa Oktoba 11, 2018 akibainisha kuwa alipigiwa simu leo alfajiri Oktoba 20, 2018 akielezwa kuwa amepatikana


Dar es Salaam. Gullam Dewji Hussein, baba wa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amesimulia jinsi alivyompata mwanaye aliyetekwa Oktoba 11, 2018 akibainisha kuwa alipigiwa simu leo alfajiri Oktoba 20, 2018 akielezwa kuwa amepatikana.

Akizungumza na MCL Digital, Gullam amesema alijulishwa kuwa mwanaye amepatikana akiwa katika gari ambalo lilitelekezwa katika viwanja vya Gymkhana jijini hapa.

Amesema Mo Dewji baada ya kushushwa katika gari hilo alitembea kutafuta msaada wa simu.

Amebainisha kuwa baada ya kupokea simu hiyo alifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kumuona mwanaye.

“Namshukuru Mungu nimemkuta Mo akiwa salama na haraka nilimpeleka nyumbani lakini tumemkuta ana majeraha kidogo ila jambo la kushukuru ni kwamba yuko hai,” amesema Gullam.

“Tulipofika nyumbani tulianza kufanya mawasiliano na Jeshi la Polisi kwa kuwapa taarifa kuwa kijana wangu nimempata na wao (polisi) walifika nyumbani kwangu Oysterbay.”

Gullam amemshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha kupatikana kwa mwanaye.