Hatua kwa hatua tangu kutekwa kwa mfanyabiashara Mo Dewji

Muktasari:

Tangu kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ Oktoba 11, 2018 hadi leo Jumanne Oktoba 16, 2018 hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za kinachoendelea


Dar es Salaam. Oktoba 11, 2018  saa 11:30 alfajiri mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji alitekwa wakati akiwa katika Hoteli ya Colosseum Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Tangu siku hiyo hadi leo mchana Jumanne Oktoba 16, 2018  hakuna taarifa zozote za watekaji, lengo la kumteka wala fununu za alikohifadhiwa Mo Dewji ambaye miaka mitatu iliyopita jarida la Forbes lilimtaja kuwa tajiri namba moja Afrika kwa vijana walio chini ya miaka 40.

MCL Digital imekuchambulia  mambo yaliyotokea na kuzungumzwa kuhusu tukio hilo tangu lilipotokea hadi leo.

Viongozi wamiminika hotelini

Takribani saa mbili tangu Mo Dewji kutekwa askari polisi na viongozi mbalimbali walifika katika hoteli ya Colosseum.

Baadhi ya waliojitokeza ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa pamoja na maofisa kadhaa wa usalama.

Ulinzi ulikuwa mkali katika eneo hilo wakati maofisa wa polisi wakifanya uchunguzi wa awali kwa kutumia vipimo mbalimbali.

Mambosasa ataja wahusika wa utekaji

Muda mchache baada ya kufika katika eneo la tukio,   Mambosasa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Mo Dewji alitekwa na Wazungu wawili waliokuwa katika gari aina ya Toyota Surf, kwamba kulikuw ana magari mawili, moja lilikuwa ndani na jingine nje ya hoteli hiyo. Alisema wahusika walikuwa wamefunika nyuso zao.

Uvumi wazagaa Dewji amepatikana

Kuanzia saa sita mchana Oktoba 11, 2018 taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara huyo zilianza kuzagaa ikidaiwa kuwa zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda akanusha

Taarifa hizo zilikanushwa na Makonda  na kubainisha kuwa huenda waliotoa taarifa hizo walimnukuu vibaya.

Manara akamatwa na polisi

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alikamatwa na polisi kutokana na tukio la kutekwa kwa Mo Dewji kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia, jambo ambalo lilidaiwa kuwa si kweli.

Manara alikamatwa Oktoba 11 jioni na kuachiwa kabla ya kukamatwa tena Oktoba 12, 2018 asubuhi.

Lugola azungumza

Jumamosi, Oktoba 13, 2018 Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola alizungumza na vyombo vya habari na kubainisha kuwa polisi inaendelea na mchakato wa kumtafuta mfanyabiashara huyu.

Aliwaeleza wanahabari kuwa  wakati huo watu 20 walikuwa wakishikiliwa na polisi akataka ndani ya saa 24 watu wanaowashikilia kwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo mara baada ya kuwahoji na kubaini hawahusiki au hawana taarifa kamili waachiliwe.

Wanaoshikiliwa na polisi wafikia 26

Hadi kufikia Jumapili, Oktoba 14 idadi ya watu waliokuwa wakishikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio la kutekwa kwa Dewji ilifikia 26, Manara.

Jeshi la polisi lilisema hatua hiyo ni sehemu ya kazi ya uchunguzi na baada ya kukamilisha kuwahoji taarifa zaidi ingetolewa.

Masauni na CCTV

Jumapili Oktoba 14, 2018 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Serikali inatarajia kusambaza kamera maalum za CCTV katika miji mikubwa na baadhi ya mikoa ili kukabiliana na matukio ya uhalifu.

Sh1 bilioni kutolewa

Jumatatu mchana, Oktoba 15, 2018  familia ya Dewji ilitangaza donge nono la Sh1 bilioni kwa yoyote atakayefanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo  na kwamba familia hiyo imeahidi kumlinda mtoa taarifa hizo.

Familia ilitangaza namba za simu zitakazotumika kukusanya taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa bilionea huyo.

19 waachiwa kwa dhamana

Leo Oktoba 16, 2018 Mambosasa alisema watu 19 kati ya 26 waliokuwa wakishikiliwa na  polisi wakihusishwa na tukio la kutekwa mfanyabiashara huyo wameachiwa kwa dhamana, akiwemo Manara.

Soma zaidi: