Jalada la Mke wa Bilionea Msuya latua kwa DPP

Muktasari:

  • Jalada la  kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Dar es Salaam. Jalada la  kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Hayo yameelezwa leo Oktoba 8 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili Mwita amedai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, jalada bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwamba wanasubiri uamuzi wake.

Baada ya kueleza hayo, Mwita ameiomba mahakama iipangie kesi hiyo tarehe ya kutajwa ili aweze kufuatilia jalada la kesi hiyo.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba amemwambia wakili huyo wa Serikali alifuatilie jalada hilo kwa ukaribu na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22, mwaka huu.

Katika kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2017, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa marehemu bilionea Msuya aitwaye Aneth Msuya.

Tukio hilo, linadaiwa kufanywa Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam. Washtakiwa hao, awali Februari 23, 2016, waliachiwa huru katika kesi ya mauaji namba 32 ya mwaka 2016 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa.

Baada ya kufutwa kwa kesi hiyo iliyokuwa ikifanana na hii baadaye walikamatwa na kusomewa mashtaka hayo ya mauaji upya.