Bunge Newzeland kuruhusu utoaji mimba

Muktasari:

  • Ni baada ya Serikali ya nchi hiyo kuwasilisha mswada wa mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu utoaji wa mimba.

New Zealand. Wakati Tanzania utoaji wa mimba ni kosa la jinai, New Zealand inatarajiwa kufanya mabadiliko mapya ya sheria yatakayoruhusu kitendo hicho.

Mswada huo uliwasilishwa bungeni leo Jumatatu Agosti 5 unatarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza siku ya Alhamisi.

Baadaye mswada huo utapelekwa katika kamati maalum kwa ajili ya raia kutoa maoni yao kisha utawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.

Mswada huo unataja kitendo cha utoaji mimba kuwa ni suala la kiafya badala ya uhalifu na kuondoa sharti la mwanamke ambaye ana uja uzito wa chini ya wiki 20 kuchunguzwa.

Hadi sasa utoaji mimba ni kitendo cha uhalifu nchini New Zealand na ni jambo linaloweza kufanywa kwa lengo la kuokoa maisha ya mama au kuilinda afya yake ya kimwili na kisaikolojia.

Hata hivyo, ili suala hilo kufanyika ni sharti idhini itoke kwa madaktari washauri wawili.