Mwandishi atimuliwa kwa kumwalika Besigye kwenye kipindi

Kampala, Uganda. Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha redio cha Aulogo FM ya wilayani Adjumani nchini Uganda, Williams Anyama amemfukuza kazi meneja mtangazaji Amacha Golo kwa kumwalika kwenye kipindi Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dk Kiiza Besigye.

Katika barua yake ya Julai 6, Anyama alimwagiza meneja wa kituo hicho kuwasilisha barua yenye maelezo ya kina kuhusu mazingira ambayo redio hiyo ilipanga kumwalika Dk Besigye na maofisa wengine, kabla ya kipindi hicho kuzuiwa na maofisa usalama na kukiweka kituo hicho katika hali tatanishi. 

“Kwa nakala ya barua hii, wewe (Amacha) unaagizwa kuwa nje ya ofisi ili kupisha uchunguzi wa suala hilo na unatakiwa kukabidhi ofisi kwa meneja wa vipindi mara moja. Utataarifiwa baada ya kupata maelezo na kufanya uchunguzi wa suala lenyewe,” barua iliyonukuliwa na Gazeti la Daily Monitor inaeleza.
Meneja wa kituo hicho, Julius Asiimwe alisema wamechukua hatua hiyo ili kutuliza munkari wa baadhi ya wafuasi wa chama cha NRM, wanaodhani kuwa vyombo vya habari vinawapatia nafasi kubwa viongozi wa upinzani kutoa maoni yao.

“Tulipokea na kutoa stakabadhi ya fedha Sh1.6 milioni kwa ajili ya kipindi hicho cha saa 2. Nilitakiwa kumfahamisha mkuu wa wilaya na kamanda wa polisi wa wilaya kuhusiana na masuala ya kiusalama, nikafanya hivyo na baadaye polisi na wanajeshi wakakizingira kituo na kukizuia kipindi.

Akizungumza na Daily Monitor, Goli alisema: “Barua imeandikwa kwa haraka na hisia kali na mwanasiasa mwenye hofu. Mimi sihusiki na vipindi. Sielewi, kwa nini lawama za kushindwa kwa menejimenti zinaweza kutupwa kwangu. Hii ni kutafuta mchawi katika siasa. Hata kama, kipindi baadaye kilifutwa na mimi sikuwa mwenyeji wake. Sikufahamu kuhusu kipindi chenyewe,” alisema.

Aliongeza: “Kuna tatizo gani kumkaribisha Besigye, rais wa zamani wa DCP katika kipindi cha redio? Hili ni jaribio la kuzuia uhuru wa vyombo vya habari katika Adjumani ili kuirudisha katika chama kimoja. Hii ni kinyume na maadili na taaluma kwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wanalazimishwa kufanya kazi za uofisa uhusiano.”

“Tunaziomba taasisi za haki za binadamu na za kisheria kuisaidia kukiokoa kioo cha jamii yetu, ambayo sasa inaharibiwa na wanasiasa wanaomiliki hizi redio na wanataka kucheza muziki wao,” alisema.

Dk Besigye alisema: Serikali haina ufafanuzi kutuondoa kwenye vituo vya redio. Wanaharibu biashara ya radio. Tulilipa Sh1.6 milioni kwa kipindi cha saa mbili. Hii pia tulizozwa kiasi kikubwa ili kutuzuia, lakini tulilipa. Ajabu polisi walikuja na kutuzuia. Hata hivyo tutaendelea kupigania haki zetu.

Hata hivyo, si mara ya kwanza Besigye kuzuiwa katika vituo vya redio. “Muda mrefu zaidi kwangu kuzungumza katika vituo vya redio nilivyotembelea ni dakika 15 tu. Na hii ni pale usipotangaza. Hii inafanywa na awamu iliyochanganyikiwa, ambayo haitaki kushawishi watu na rasilimali, alisema Besigye.

Machi 2016: Vyombo vya habari vilitakiwa kutangaza kutokea nyumbani kwa mwanasiasa huyo, Kasangati lakini vilizuiwa.
Vilevile, Aprili mwaka huu polisi katika wilaya ya Mubende walivamia Kituo cha Radio cha Mubende FM na kukizima ili mwanasiasa huyo asikitume kuzungumza.

Pia Aprili 13 na Aprili 4, vituo vya Kiira FM cha Jinja na Hope cha Manispaa Kabale pia vilizimwa kumzuia.