Trump athibitisha wahamiaji kusakwa, kurejeshwa kwao wikiendi hii

Muktasari:

Inasadikiwa kuwa Marekani ina wahamiaji wapatao milioni 10.5 ambao hawana nyaraka halali za kuishi katika taifa hilo tajiri duniani.

Rais wa Marekani, Donald Trump amethibitiosha kuwa mawakala wa idara ya uhamiaji wataanzisha msako nchi nzima mwishoni mwa wiki hii kusaka maelfu ya watu wanaoishi isivyo halali kwa ajili ya kuwarejesha makwao.

"Wanakuja isivyo halali," aliwaambia waandishi wa habari Ikulu. "Watawachukua (majumbani mwao) na watawasafirisha kurudi kwenye nchi zao."

Trump alisema maofisa hao wa uhamiaji wataangalia zaidi watu ambao wana rekodi za uhalifu, kama walio katika makundi ya wahuni lakini pia na wengine.

"(Msako) Unaanza Jumapili wa kuwaondoa wahalifu (nchini) na watu watatolewa nje na watawasafirisha kurudi kwenye nchi zao," alisema Trump alipoongea na waandishi Ikulu.

"Ama watawaondoa wahalifu au watawaweka katika magereza ya nchi wanazotoka."

Wakati watawaangazia zaidi wahalifu, Trump alisema msako huo wa uvamizi pia utawaangazia "watu wanaokuja kwenye nchi yetu si kwa kufuata utaratibu, ambao huja tu. Nao wanatakiwa waondoke."

Msako huo unatarajiwa kufanyika katika miji kumi mikubwa, ukielekeza nguvu kwa watu ambao mahakama zimeshatoa amri za kuwaondoa, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

Maofisa hao wa uhamiaji wanawaeza kuangalia zaidi familia ambazo zimeishi Marekani kwa muda mrefu, zikiwa na makazi, biashara na watoto waliozaliwa katika taifa hilo kubwa kiuchumi ulimwenguni.

Kwa mujibu wa taasisi ya Pew Research Center, kuna takriban wahamiaji milioni 10.5 wasio na nyaraka zinazotakiwa nchini Marekani na theluthi mbili wamekuwa wakiishi nchini humo kwa zaidi ya miaka 10.

Ken Cuccinelli, kaimu mkurugenzi wa kitengo cha huduma na uraia cha idara ya uhamiaji, alisema Jumatano kwamba maofisa wa ICE wameshapewa amri ya kuwaondoa nchini Marekani wahamiaji milioni moja, lakini akaongeza kuwa chombo hicho hakina vifaa na wafanyakazi wa kutosha kuwakamata na kuwarejesha kwao.