Meneja ashikwa kigugumizi kwa waziri

Friday January 25 2019Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa 

By Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Kongwa. Meneja wa Mamlaka ya Maji mji mdogo wa Kibaigwa wilayani hapa mkoani Dodoma, Boniface Bihemo ameshikwa kigugumizi kumweleza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa idadi ya uniti anazotumia mwananchi wa kawaida kwa siku.

Hali hiyo ilitokea juzi wakati wa ziara ya waziri huyo ya kuangalia changamoto zinazoikabili sekta ya maji wilayani Kongwa.

Baada ya kushindwa kueleza matumizi ya mwananchi wa kawaida, Profesa Mbarawa alimhoji meneja huyo uniti anazotumia nyumbani kwake kwa siku lakini pia alishindwa kutaja.

“Kama mwenyewe hujui unatumia uniti ngapi kwa siku itakuwa vigumu kujua wananchi wanatumia maji kiasi gani,” alisema.

Awali, Bihemo alisema mji wa Kibaigwa una wakazi zaidi ya 2,000 na kwa siku wanazalisha lita 1,200 za ujazo na wanakusanya Sh36 milioni kwa mwezi.

Alisema matumizi ya umeme ni kati ya Sh10 milioni na Sh12 milioni pamoja na matumizi mengine wanabakiwa na Sh5 milioni.

Advertisement

Hata hivyo, mbunge wa jimbo hilo, Job Ndugai alisema kitendo cha meneja huyo kushindwa kueleza uniti za maji anazotumia, inaonyesha halipii maji.

“Waliopewa fursa ya kuendesha miradi ya maji ndiyo wenye tatizo siyo Serikali, kwani wanashindwa kuisimamia vyema hivyo tunaomba uivunje bodi ya mamlaka hii kwa kushindwa kuwajibika,” alisema Ndugai ambaye pia ni Spika wa Bunge.

Baada ya maelezo hayo, Profesa Mbarawa aliivunja bodi hiyo iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake, Simon Mitumba.

Profesa Mbarawa alisema kama bodi ingefanya kazi vizuri mamlaka hiyo ingekusanya zaidi ya Sh52 milioni badala ya Sh36 milioni za sasa.

Advertisement