Nyaraka KKKT, TEC zilivyoibua mijadala

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo

Muktasari:

  • Akizungumza Desemba 9 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 34 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki ya Pwani (DMP). Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema taasisi za dini na viongozi wanapaswa kuhimiza upendo na mshikamano pamoja na kuliombea Taifa ili Watanzania waendelee kuishi kwa amani na utulivu.

Dar/Moshi. Siku nane zimebaki kuufunga mwaka 2018 na kuingia 2019. Kama ilivyokuwa kwa miaka mingine, 2018 umekuwa na milima na mabonde mengi na mambo kadha wa kadha yamejitokeza, ikiwa ni pamoja na taasisi na jumuiya za kidini kuzungumzia masuala mbalimbali ya nchi, huku wakati mwingine wakitoa ujumbe kupitia nyaraka.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu walitoa nyaraka katika vipindi tofauti zilizokosoa masuala mbalimbali serikalini na katika jamii.

Mbali na kuzungumzia masuala ya kiroho, waraka wa KKKT ulitaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini wake “ili waongeze mzigo wa kuliombea Taifa letu na viongozi wake.”

Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la “Taifa Letu, Amani Yetu” na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo la Katiba Mpya.

Katika waraka wa TEC uliotolewa na maaskofu wote 35 wakiongozwa na Rais wake, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa uliopo katika kitabu cha kurasa 20, kanisa hilo lilitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Juni 2018, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nao walitoa waraka wa salamu za Sikukuu ya Eid el-Fitr uliokuwa umebeba mambo manane.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu waraka wao, Mkuu wa KKKT, Dk Frederick Shoo alisema ujumbe walioutoa kwa Taifa kupitia waraka wa Pasaka, kwa kiasi fulani umepokewa na kusisitiza kuwa kuna haja ya waraka ule kuendelea kufanyiwa kazi kwa manufaa ya jamii.

“Tunazidi kusisitiza kuwa yale mambo tuliyoyasema kwenye waraka wa Pasaka yaangaliwe kwa makini na yatafakariwe. Wenye kuhusika waendelee kuyafanyia kazi kwa manufaa ya jamii yetu,” alisema Dk Shoo.

Waraka wa KKKT

Machi 24, KKKT lilitoa waraka uliozungumzia hali ya kiuchumi, ukipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kukusanya kodi, umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika mikakati ya maendeleo, utawala bora, demokrasia ya vyama vingi, usalama wa raia na masuala mengine mtambuka.

Waraka huo uliosainiwa na maaskofu 27, ulichagiza kutengwa kwa maaskofu watatu wa kanisa hilo huku maaskofu wengine wakiomba radhi kwa kutosoma waraka huo makanisani.

Siku tatu baada ya waraka huo, Rais John Magufuli aliwataka viongozi wa dini kuiombea Tanzania ya viwanda ili kuongeza ajira na kuokoa mabilioni ya fedha zinazopotea, lakini Makamu wa Rais, Samia Suluhu akitoa wito kwa viongozi wa dini, akiwataka kuikosoa Serikali kwa lugha watakayoelewana.

Waraka huo uliibua makundi mbalimbali ya wanasiasa, wananchi na wasomi waliopinga na kuunga mkono huku barua ya Serikali iliyowataka maaskofu hao kutengua tamko hilo ndani ya siku 10 ikinogesha mjadala zaidi mtaani, mitandaoni na ndani ya Bunge.

Barua hiyo ilisambaa mtandaoni ikiwa imesainiwa na mtu aliyeitwa M. Komba, kwa niaba ya msajili wa Vyama vya Hiari Wizara ya Mambo ya Ndani.

Hata hivyo, Dk Shoo alinukuliwa akisema kanisa halikukurupuka kuutoa waraka huo wa Pasaka na ulitolewa kwa washarika wa kanisa hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Dk Mwigulu Nchemba alisema barua hiyo ilikuwa ni batili kisha akatangaza kumsimamisha msajili wa taasisi za kijamii, Merlin Komba, ambaye alirejeshwa tena kazini siku 24 tu baada ya Mwigulu kutumbuliwa.

Kitendo cha Serikali kuagiza maaskofu kufuta waraka huo ndani ya siku 10 kiiibua mjadala na maswali ndani ya Bunge, Juni 8, huku Naibu Spika Dk Tulia Ackson akimzuia Waziri Mkuu kujibu swali lililohusu barua hiyo ya Serikali. Vyama vya upinzani vililitaka kanisa hilo kutoijibu barua ya Serikali.

Dk Shoo alipoulizwa kama waliyoyaeleza katika waraka huo yamefanyiwa kazi, alisema, “Miongoni mwa mambo yaliyofanyiwa kazi ni matukio ya watu kutoweka pamoja na mambo ya haki za binadamu, kwa kiasi fulani yalipokewa na tumeona yamefanyiwa kazi”.

“Tunaona yale mambo ya mashambulizi pia yamefanyiwa kazi na yamepungua na ni ngumu ku-judge (kuhitimisha) kuwa yametekelezeka mia kwa mia, lakini yapo mambo ambayo yamefanyiwa kazi kwa kiasi na yanaendelea kufanyiwa kazi.”

Waraka wa TEC

Februari, TEC walitoa ujumbe wa Kwaresma wa 2018 kwa waumini wao na ndani yake ulieleza msimamo wa maaskofu 35 wa kanisa hilo. Licha ya kuwa na ujumbe wa masuala ya koroho, waraka huo ulizungumzia hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kisiasa, ulisema uamuzi wa Serikali kuzuia maandamano, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni kwenda kinyume na Katiba ya nchi. Pia ulionya Serikali kutovibana vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuvifungia kwa sababu mbalimbali, kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge.

Kiuchumi, uligusia suala la kodi na katika masuala ya kijamii ukieleza kuwa bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii.

Waraka huo uliwagawa makundi maaskofu wa kanisa hilo, huku Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo akisema hakuwa na taarifa za kutolewa kwa waraka huo wa Kwaresma na TEC akibainisha kuwa waraka huo una mazuri mengi japo umechanganya dini na siasa.

Jumuiya na Taasisi za Kiislamu

Juni 17, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ilitoa waraka wa salamu za Eid el-Fitr, uliokuwa umebeba mambo manane yakiwamo masuala ya haki na uhai, uhuru wa habari na kujieleza, wa Bunge na Mahakama, wa kisiasa na Katiba Mpya.

Waraka huo wa kurasa tisa ulisomwa na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda katika Msikiti wa Mtambani uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Sheikh Ponda alisema kutokana na matukio yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka haki ya kuishi, uhuru wa habari na kujieleza vimeanza kutoweka kupitia matukio ya kuokotwa kwa miili ya watu ufukweni na kanuni mpya katika sheria ya habari zinapaswa kubadilishwa.

Waraka huo pia ulikemea mazingira ya ubaguzi wa vyama vya siasa kushiriki katika siasa, kupungua kwa uhuru wa Bunge, kukosekana kwa haki na uhuru wa kuchagua viongozi kupitia Tume ya Taifa ulioitaja kuwa isiyokuwa huru huku wakipendekeza kuanzisha mjadala wa kitaifa wa kikatiba ili kupata muafaka.