Rufaa dhamana ya Mbowe, Matiko kusikilizwa Februari 18

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimiana na mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, Mbowe na wenzake nane walifika mahakamani hapo kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.  Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Leo Alhamisi Januari 31, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa rufaa ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka dhidi ya Freeman Mbowe na Ester Matiko itaanza kusikilizwa  Februari 18, 2019


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  imeelezwa kuwa rufaa ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka dhidi ya Mwenyekiti wa  Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko itaanza kusikilizwa  Februari 18, 2019  katika Mahakama ya Rufaa.

Taarifa hiyo umetolewa leo Alhamisi Januari 31, 2019 na wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wankyo amedai kuwa kesi lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa.

"Washtakiwa wote wapo  mbele ya mahakama yako na kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuna rufaa iliyopo mahakama ya rufaa ambayo bado haijasikilizwa, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa, wakati tukisubiri maamuzi ya mahakama ya rufaa,” amedai Wankyo.

Amedai kuwa rufaa hiyo ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka itaanza kusikilizwa  Februari 18, 2019.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari akisaidia na Hekima Mwasipu walikubaliana na hoja za upande wa mashtaka.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza hoja za pande zote , ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 14, 2019 itakapotajwa.

Hata hivyo, Mbowe na Matiko ambaye pia ni mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) wanaendelea kusota rumande kutokana na kufutiwa dhamana.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana zao  Novemba 23, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri  ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Kibamba, John Mnyika; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji;  mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wengine ni naibu makatibu wakuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara); mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza tangu Mbowe na wenzake wafikishwe mahakama ya Kisutu, leo aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu ameonekana mahakamani kufuatilia kesi hiyo.