Hivi ndivyo Hakimu alivyowapa dhamana wabunge wa Chadema, wenzao

Wakili hekima Mwasipu akisikiliza jambo kutoka kwa wabunge wa Chadema, Peter Lijualikali kushoto na mbunge wa jimbo la Mlimba, Suzani Kiwanga baada ya mahakama ya hakimu mkazi Morogoro kutupilia mbali pingamizi la jamhuri la kuzuia dhamana la wabunge hao na wenzao saba katika kesi ya jinai inayowakabili washtakiwa hao leo. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

Kiwanga, Lijualikali na wenzao saba wapewa dhamana, mahakama yatupilia mbali maombi ya upande wa mashataka kupinga dhamana  


Morogoro. Wabunge wa Chadema, Suzan Kiwanga (Mlimba), Peter Lijualikali wa Kilombero na wenzao saba wamepata dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kutupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka ya kupinga dhamana yao.

Wabunge hao pamoja na wenzao, wamepata dhamana baada ya kusota rumande kwa takriban wiki mbili tangu walipofikishwa mahakamani hapo.

Wabunge hao na wenzao wapewa dhamana baada ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Elizabert Nyembele, anayesikiliza kesi hiyo kupitia hoja za upande wa mashtaka za kupinga dhamana na zile za upande wa utetezi zilizoeleza upungufu ya maombi hayo.

Kabla ya kufikia uamuzi wa kuwapa dhamana hakimu Nyembele ameieleza mahakama kuwa maombi yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka yana upungufu ambao hauwezi kurekebishika. Pia, hayana nguvu ya kisheria mbele ya mahakama hiyo.

Nyembele ameeleza mazingira ya kesi hiyo hayamruhusu wala hayamsukumi kutumia mamlaka ya mahakama kupinga dhamana ya washtakiwa hao hivyo ametupilia mbali maombi hayo ya upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Machi 22, 2019.

Hata hivyo, Nyembele amesema lazima washtakiwa hao wakidhi masharti ya dhamana kwa kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayewasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sio chini ya Sh5 milioni na atakayeweza kutoa dhamana ya Sh3,756,000.

Baada ya kupewa dhamana wabunge hao na washtakiwa wenzao walijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na wadhamini waliojiandaa kutokuwa na hati ya mali zisizohamishika zenye hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Devota Minja ambaye amefika mahakamani akiwa na wafuasi wengine wa chama hicho alionekana kuhangaika ili kupata wadhamini wenye sifa huku akiwahakikishia washtakiwa hao kuwa watadhaminiwa kabla ya Mahakama kufungwa.

Wabunge hao na wenzao saba wanashtakiwa kwa kesi ya jinai namba 43 ya mwaka 2019 na kwamba Novemba 26, 2017 walitenda makosa nane likiwamo la kuharibu mali na kuchoma  ofisi ya serikali ya kijiji cha Sofi wilaya ya Malinyi.

Awali, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na wakili wa Serikali mwandamizi Neema Haule, uliwasilisha maombi ya kupinga dhamana kwa madai taratibu za kisheria za kupinga dhamana ya washtakiwa hao zimefuatwa na wametumia kifungu cha sheria namba 392 A cha mwenendo wa makosa ya jinai.

 Naye wakili upande wa utetezi Hekima Mwasipu aliwasilisha hoja za kupinga zuio hilo la dhamana akidai kuwa halikufuata taratibu za kisheria hivyo sio halali.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kama washtakiwa hao wamekidhi masharti ya dhamana