Tiba asili za barabarani zapigwa marufuku Iringa

Muktasari:

Shirikisho la vyama vya tiba asili Tanzania,  limepiga marufuku waganga wa tiba za asili kufanya shughuli zao barabarani na kwenye nyumba za kulala wageni ili kuepusha udanganyifu na vitendo vya uhalifu kama ubakaji na mauaji.

Iringa. Shirikisho la vyama vya tiba asili Tanzania,  limepiga marufuku waganga wa tiba za asili kufanya shughuli zao barabarani na kwenye nyumba za kulala wageni ili kuepusha udanganyifu na vitendo vya uhalifu kama ubakaji na mauaji.

 Hayo yamesemwa jana Jumatano Juni 26, 2019 na Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya tiba asili Tanzania,  Abdulrahman Lutenga  katika  mkutano na waganga wa tiba asili na Polisi wa mkoani Iringa .

Lutenga amesema ni jukumu la kila mmoja kushiriki  kuwafichua waganga hao kwa sababu madhara ya kuwahifadhi ni makubwa na yanasababisha mauaji na ubakaji wa watoto.

“Naomba wananchi watoe taarifa kwenye vyombo husika kama watawabaini waganga wanaopiga ramli kwa sababu ndiyo  wanatuhumiwa kuchochea mauaji ya vikongwe, watoto, watu wenye ualbino, ubakaji na utapeli,” amesema Lutenga.

Amesema waganga wote wanaotoa huduma ya dawa za asili barabarani na kwenye mikusanyiko ya watu hawatambuliwi na shirikisho la Waganga wa Jadi.

 Kwa upande wake Mkuu wa upelelezi Mkoani Iringa, Juma Seleman aliwaasa waganga kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu bali wanapaswa kuisaidia Serikali kuwanasa wahusika wa matukio hayo, wakiwamo majambazi ambao huenda kusaka kinga kwao.

Amesema kumekuwapo na matumizi ya nyara za Serikali kwa kisingizio cha dawa kinyume cha utaratibu na ni kosa la jinai.

“Serikali haijawahi kusajili washirikina na waganga, hivyo tunawaomba mfanyekazi  kwa kuzingatia utaratibu na sheria ya tiba asili kama inavyowataka.

 “Nawaomba  wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona kuna mganga mgeni katika maeneo yao ili kuwapata waganga feki ambao wanachangia uhalifu wa mauaji,” amesema Seleman.