VIDEO: Alichokisema Mbowe kabla ya kwenda mahabusu

Alichokisema Mbowe kabla ya kwenda mahabusu

Muktasari:

Mwenyekiti huyo wa Chadema pamoja na viongozi wengine wa chama hicho kikuu cha upinzani wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko isivyo halali, kutotii tamko la kuwataka watawanyike na kusababisha vurugu.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kuwa “imara na kutoogopa” akisema kesho ni “nzuri kuliko jana” baada ya kufutiwa dhamana yake.

Mbowe alitoa kauli hiyo, akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo (Ijumaa Novemba 23, 2018), baada ya mahakama hiyo kumfutia dhamana na mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko kwa kukiuka masharti ya dhamana hiyo.

Mbali na Mbowe, wengine katika rufaa hiyo ni Dk Vicent Mashinji (katibu mkuu), John Mnyika (naibu katibu mkuu Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar), Ester Bulaya (mbunge Bunda), John Heche (Tarime Vijijini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Halima Mdee (Kawe).

Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alitumia kizimba cha mahakama hiyo kusalimiana na viongozi wengine wa Chadema na wafuasi pamoja na kutoa ujumbe wake wa kuwatia moyo.

 “Naomba muwe stable (imara), msiogope. Kesho ni nzuri kuliko jana,” alisema Mbowe kisha akamalizia na salamu ya chama hicho ya “peoples” na wafuasi kuitikia “power”.

Kabla ya kutoa ujumbe huo, askari walitaka kumuondoa katika kizimba, lakini akawasihi akisema “kwanza nizungumze na watu wangu”.

Uamuzi wa kuwafutia wawili hao dhamana ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri akisema kitendo kilichofanywa na washtakiwa hao ni kudharau amri za mahakama kwa makusudi.