Bodaboda auawa kwa kupigwa na abiria

Muktasari:

Polisi mkoani Morogoro inamsaka mtu mmoja ambaye anatuhumiwa kumpiga kichwani mwendesha bodaboda hali iliyosababisha kupoteza maisha


Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamsaka mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi kwa tuhuma za kumuua dereva bodaboda Salumu Ramadhan (40).

Tukio hilo lilitokea Jumatatu ya Januari 7, 2019 majira ya saa nne usiku eneo la Foren Pub - Mawenzi katika Manispaa ya Morogoro ambapo mtuhumiwa alimpiga bodaboda huyo kichwani baada ya kukataa kumpakia mwanamke  aliyekuwa naye kwenye pikipiki kwa nauli ya Sh500.  

Akizungumzia mauaji hayo leo Alhamisi Januari 10, 2019,  kaka wa marehemu, Juma Kijoka amesema ndugu yake alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kabla ya kupatiwa matibabu na alizikwa jana kijiji cha Mikese, Wilaya ya Morogoro. 

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo bado hajakamatwa huku akiwataka watu wenye taarifa zake kuzitoa kwa Jeshi la Polisi ili waweze kumkamata na kumchukulia hatua za kisheria.