Jaji Kiongozi Tanzania atoa maagizo kwa majaji, mahakimu

Monday July 22 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jaji Kiongozi wa Tanzania, Dk Eliezer Feleshi ametoa waraka maalumu wenye maelekezo yanayolenga kufanyia kazi maelekezo ya Rais wa nchi hiyo, John Magufuli kuhusu kukabiliana na tatizo la msongamano wa mahabusu katika magereza.

Julai 17, 2019, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika gereza la Butimba, Mwanza na kushuhudia changamoto nyingi  ikiwamo msongamano wa mahabusu huku wengine wakiwa wamekaa muda mrefu bila kupelekwa mahakamani na wengine kwa kesi za kubambikiwa.

Hivyo,  Rais Magufuli alitoa maelekezo kwa Wizara ya Katiba na Sheria na vyombo vingine vinavyosimamia utoaji wa haki nchini kuchukua hatua stahiki kumaliza matatizo hayo.

Jaji Kiongozi, katika waraka wake namba nne wa mwaka 2019 kwenda kwa majaji wasajili na mahakimu kuchukua hatua mbalimbali zitakazosaidia kuondoa tatizo hilo huku akisisitiza utoaji wa adhabu mbadala, badala ya adhabu za vifungo jela.

Waraka huo wa Julai 19, 2019 Mwananchi limeuona na jana Jumapili Julai 21, 2019 ulithibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Mahakama ya Tanzania, Nurdin Ndimbe alipoulizwa na Mwananchi.

Waraka huo umeelekezwa kwa majaji wafawidhi  kanda zote 16 za Mahakama Kuu Tanzania na Divisheni za Mahakama Kuu, yaani Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Divisheni ya Ardhi, Divisheni ya  Biashara na Divisheni ya Kazi.

Advertisement

Pia umelekezwa kwa Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo, kwa ajili ya utekelezaji wa maelekezo hayo.

Jaji Kiongozi katika waraka huo amewasisitiza watendaji hao wa mahakama kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya kisheria yanayoelekezwa katika sheria mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo.

Baadhi ya matakwa hayo ya kisheria ameyataja ni pamoja na  haki ya mtuhumiwa/mshitakiwa kupata maelezo ya mlalamikaji pamoja na hati ya mashtaka pale kesi inapofunguliwa mahakamani;

 

Mengine ni kutolewa kwa dhamana polisi kwa makosa yanayodhaminika pale ambapo polisi hawajakamilisha upelelezi na kutolewa kwa dhamana mahakamani kwa makosa yanayodhaminika kwa kufuata vigezo vya kisheria baada ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani, isipokuwa kwa maslahi ya umma kwa misingi ya sheria.

Vilevile Jaji Kiongozi amewakumbusha majaji na mahakimu kuwa sheria inawataka kutoa hukumu ndani ya siku 90 kuanzia siku ya usikilizwaji wa kesi ulipokamilika, huku akiwataka wapelelezi na waendesha mashtaka kuzingatia mwongozo wa Serikali kutokufungua kesi kabla ya kukamilisha upelelezi.

“Kwa upande wa wapelelezi na waendesha mashtaka ni vema mfahamu Tangazo la Serikali Na. 296 la 2012 linatoa mwongozo kwa kesi nyingi isipokuwa zile zinazohusisha makosa makubwa wa kukamilishwa kwa upelelezi kabla ya kufunguliwa kwa kesi mahakamani,” unasomeka waraka huo  

“Aidha, yapo Maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Novemba 3, 2008 ambayo kupitia kipengele cha 4 yanaitaka Mamlaka husika kumwajibisha mwendesha mashtaka au mpelelezi ambaye kwa hila atasababisha haki kutotendeka,” unaongeza 

Sambamba na hatua hiyo, pia Jaji Kiongozi amewataka majaji na mahakimu kushiriki  vikao vya Jukwaa la Haki Jinai na vya kusukuma kesi ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa. 

Amebainisha  vikao hivyo ni nyenzo za kuziwezesha mamlaka zinazohusika na utoaji wa Haki Jinai kutatua changamoto zinazojitokeza katika ngazi mbalimbali katika nchi yetu.

Pia, katika kukabiliana na matatizo hayo, ametoa maelekezo kwa majaji na mahakimu kwa nafasi zao kuchukua hatua sita ambazo ni pamoja na kuhakikisha kesi zinazofikishwa mahakamani zina kidhi matakwa ya kusajiliwa kisheria.

 “Na zinaposajiliwa hakikisheni mienendo hiyo inaendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria ambayo baadhi yametajwa hapo juu,” amesisitiza Jaji Kiongozi.

Hatua nyingine ni kuhakikisha kesi zinasikilizwa na kutolewa hukumu/uamuzi katika muda uliowekwa na sheria na kwa kuzingatia malengo ya Mahakama na kuhakikisha fursa za adhabu mbadala ya kifungo cha jela inapewa kipaumbele kwa kufuata sheria;

 Nyingine ni kuhakikisha vikao vya kusukuma kesi vinafanyika kadri ya Waraka wa Jaji Mkuu Na.2/1987 kama ulivyorekebishwa. mwaka 2003 na 2011 na wachukue  hatua zinazostahili kutekeleza maazimio yake, ambavyo Mahakimu Wafawidhi, Naibu Wasajili na Msajili Mahakama Kuu ndio wenyeviti wake.

“Hakikisheni Mahakama inashiriki kikamilifu kwenye vikao vya Jukwaa la Haki Jinai ngazi zote na hakikisheni mwongozo wa ukaguzi unafuatwa kama ulivyo ikiwa ni pamoja na kuwafichua watumishi wa mahakama watakaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa,” amesisitiza.

 Pamoja na hatua hizo pia Jaji Kiongozi amewataka majaji na mahakimu kutumia mamlaka asili ya waliyo nayo kuondosha mashtaka kumwachia huru mshitakiwa endapo watajiridhisha kuwepo kwa vitendo vya hila vinavyohujumu mwenendo wa kesi iliyo mbele.

Advertisement