Jaji Rumanyika alivyowarudishia dhamana Mbowe, Matiko

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe baada ya kuachiwa huru katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Leo Alhamisi, Machi 7, 2019 Mbowe na Matiko wamerudi tena uraiani baada ya kukaa gerezani kwa miezi mitatu kutokana na kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu


Dar es Salaam. Hatimaye Mwenyekiti wa (Chadema), Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko, wameachiwa huru kutoka mahabusu ambako wamekuwa wakishiliwa kwa zaidi ya miezi mitatu.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro na Matiko ambaye ni mbunge wa Tarime mjini, wamekuwa mahabusu katika gereza la Segerea kwa muda huo baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Hata hivyo leo Machi 7, 2019, Mahakama Kuu imewarejesha uraiani baada ya kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu wa kuwafutia dhamana na badala yake imewarejeshea dhamana hiyo, baada ya kushinda rufaa waliyoikata wakipinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu.

Hukumu hiyo ya kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu na kuwarejeshea dhamana yao wabunge hao imetolewa na Jaji Sam Rumanyika aliyesikiliza rufaa yao hiyo.

Akisoma hukumu hiyo leo Alhamisi, Machi 7, 2019 Jaji Rumanyik amesema Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana warufani hao kwani haikufuata misingi na matakwa ya kisheria.

Jaji Rumanyika amesema ni msingi wa kisheria kwamba kufutwa kwa dhamana ya mshtakiwa huja baada ya mahakama kutwaa fungu la dhamana ya mshtakiwa (bondi ya kiwango fulani ambacho mdhamini husaini kwa niaba ya mshtakiwa) endapo mshtakiwa ataruka dhamana.

Amefafanua kwamba kabla ya mahakama kumfutia mshtakiwa dhamana lazima kwanza mdhamini apewe nafasi ya kujieleza ni kwa nini fungu lake la dhamana lisitwaliwe na baada ya kutwaa fungu hilo la dhamana la mdhamini kama mshtakiwa hataonekana mahakamani basi ndipo mahakama inaweza kumfutia dhamana mshtakiwa.

“Kwa kuwa katika shauri hili wadhamini hawakuwa kutoa sababu ni kwanini fungu lao la dhamana lisitwaliwe si tu uamuzi huu wa kuwafutia dhamana warufani siyo sahihi lakini pia ulitolewa kabla ya wakati,” amesema Jaji Rumanyika na kuongeza:

“Ninaamuru warufani waachiwe huru mara moja isipokuwa kama wataendelea kushiriliwa kisheria kwa sababu nyingine. Na ninaamuru jalada la kesi hii lirudishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mara moja ili kesi ya msingi iweze kuendelea kwa haraka sana.”

Mbowe na Matiko walikata rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana, kwa sababu za kushindwa kufika mahakamani hapo bila sababu za msingi kwa ajili ya kesi yao ya jinai inayowakabili mahakamani hapo wao na viongozi wengine saba wa chama hicho.

Walifutiwa dhamana hiyo na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Novemba 23, 2018, lakini siku hiyohiyo kupitia kwa wakili wao Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu chini ya hati ya dharusa sana, wakipinga uamuzi huo.

Siku ya usikilizwaji wa dhamana yao hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliweka pingamizi la awali akiiomba mahakama hiyo isiisikilize rufaa hiyo pamoja na mambo mengine akidai kuwa haina mamlaka kwa kuwa rufaa hiyo ilikuwa inakiuka matakwa ya sheria.

Jaji Sam Rumanyika alitupilia mbali pingamizi hilo la DPP badala yake akaamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo ya kina Mbowe, lakini kabla ya kuanza kuisikiliza, DPP akakimbilia Mahakama ya Rufani kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu kukubali kusikiliza rufaa hiyo.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika hukumu yake baada ya kusikiliza rufaa hiyo, ilitupilia mbali rufaa ya DPP na kuamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo ya Mbowe.

Rufaa hiyo ya kina Mbowe ilisikilizwa jana Jumatano, Machi 6, 2019 na Jaji Rumanyika ambapo mawakili wa pande zote walitoa hoja zao na baada ya kusikiliza hoja hizo za pande zote ndipo Jaji Rumanyika alipanga kutoa hukumu yake leo Alhamisi, Machi 7, 2019.